Wakati virusi vya corona vinavyoeneza homa kali ya mapafu vikiendelea, bado wakuu wa usimamizi wa soka na klabu wanatafakari jinsi ya kumaliza msimu wa soka wa 2019/2020 ambao umegota.
Kumaliza msimu lazima busara itumike, maana itakuwa bure kuumaliza msimu kwa maana ya kuhitimisha tu, bali lazima mambo kadhaa yazingatiwe ili kuwe na tija, bingwa na wanaoshuka daraja na wale wanaopanda wapewe haki.
Watu ‘wanaopiga pesa’ ndio wanang’ang’ania kwamba mechi zianze haraka iwezekanavyo, ili kuona kwamba matakwa yao yanatekelezwa na kampuni za televisheni zenye haki za matangazo zinaachia fedha hizo.
Bila shaka neno limeshawafikia Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) kwamba kwa sasa watu wanateseka majumbani na hospitalini kwa sababu ya Covid-19 na kipaumbele chao, kwa namna yoyote ile hakiwezi kuwa ni kurejea kwa soka kwenye nchi zao au katika ngazi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) na Ligi ya Europa.
Utu unaelekeza kwamba kwanza izingatiwe uzima wa watu, afya ya watu na maendeleo yao kisha ndipo soka na biashara yake irejee na si vinginevyo. Bado watu wamefungiwa ndani, wakiwa hawaruhusiwi kuwa kwenye mikusanyiko ili kukwepa athari ya ugonjwa huu unaoua sana, hivyo kufikiria kurudi uwanjani si mwafaka.
Wapo waliotoa maoni kwamba hata sasa wachezaji, waamuzi, makocha, maofisa na wafanyakazi watakaotakiwa kuwa uwanjani wapimwe na wale wasiokuwa na Corona warudi uwanjani na kucheza bila washabiki, ikikadiriwa kwamba ni watu 300 kwa mechi moja, na zipo jumla ya mechi zaidi ya 90 zilizobaki.
Lakini wakati hayo yakisemwa, bado kuna watu wengi katika Uingereza wanaoteseka, baadhi wakiwa wanaugua, wengine wana dalili za maradhi hayo makali na rasilimali za kuwahuduia hazitoshi, hivyo haitakuwa na maana wala mantiki kuelekeza rasilimali hizo kwenye soka.
Ni wazi kwamba haitapendeza kwa ligi kufutwa kama walivyofanya Ubelgiji na wengine, kwa sababu mshindi halali mbele ya macho ya wengi hatakuwa amepatikana, wala wa kushushwa daraja au kupanda hawatakuwa wamepatikana kihalali. Ni mwafaka zaidi kusubiri, kusogeza mbele muda wa kucheza ili kila mmoja apate haki yake.
Klabu nyingi zinapenda ligi imalizike kwa mechi zote zilizobaki kuchezwa huku washabiki wakiwapo, maana hiyo ni biashara na chanzo kikubwa cha mapato kwao, lakini kwa sasa haiwezekani. Liverpool walikuwa katika njia iliyonyooka kutawazwa mabingwa baada ya miaka 30 ya kukosa taji hilo, lakini mambo yamekwenda ndivyo sivyo.
Wakati klabu zikihangaika na hali ngumu ya uchumi, wenye haki ya matangazo ya mechi za EPL – BT na Sky walikuwa wametangaza kutengeneza faida ya pauni bilioni mbili na milioni 2, mtawalia kutokana na soka katika nyakati za karibuni na hivyo hawatakiwi kuzuia kutoa kiasi cha fedha ambacho hawajatoa kwa ajili ya kumaliza msimu.
Kila mmoja anajitoa sadaka, kuanzia kwa watu binafsi, taasisi, mashirika na hata serikali ambayo inasema hali hii mbaya huenda ikaendelea kwa wiki kadhaa kama si miezi hivyo uvumilivu na uelewa ndivyo vitu pekee vinavyotakiwa kwa sasa.
Uingereza wamekuwa nyuma katika utekelezaji wa namna ya kudhibiti maradhi haya; wenzao Ujerumani walifanya vyema, vifo vikawa vichache kabisa na walioambukizwa wakatibiwa vyema na sasa wanajipanga kurejea kwenye Ligi Kuu – Bundesliga yao.
Ni wakati wa kuendelea kusubiri, huku wachezaji wakijifua kivyao majumbani mwao na kujilinda pamoja na kuwalinda wengine, ili kuepuka madhara ya kuambukizana na kupoteza maisha ambayo ni ya thamani kubwa.
Comments
Loading…