BODI ya Ligi Kuu ya England (EPL) imesitisha michuano hiyo kwa muda hadi mwanzoni mwa mwezi ujao kutokana na kuzuka kwa ugonjwa unaosambazwa na virusi vya corona.
Ligi ya Soka ya England (EFL) walichachukua uamuzi kama huo kwa sababu kama hizo, huku soka ya Uskochi ikiwa imeahirishwa bila kuelezwa itaanza lini tena. Zilizoahirishwa pia ni mechi za Super League chini ya FA kwa wanawake.
Kutokana na uamuzi wa kuahirishwa kwa michuano mbalimbali – klabu, wafanyakazi wao na biashara zinazohusiana nazo zinakabiliana na sintofahamu kwa muda sasa.theluthi mbili ya klabu za EFL zinapoteza fedha, kwa hiyo zinategemea michango ya wamiliki.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya fedha katika soka, Kieran Maguire, anasema hali imekuwa mbaya kifedha kwa klabu na ana wasiwasi kwamba mambo yatachacha zaidi pale wamiliki watakapochoka kutoa fedha na kuamua kuacha kulipa.
“Unajua wengi kati ya wamiliki wa klabu hizi ni wafanyabiashara wa humu humu ndani wanaoendesha kampuni zao wenyewe na ni wazi nao watakuwa wakipata shida kiuchumi, na msongo kutokana na kusambaa kwa Covid-19. Huenda wakashindwa kuendelea kulipa kama kawaida wafanyakazi wao kwani wamepoteza pia oda za kibiashara au hawawezi kutimiza mikataba waliyokuwa wameingia na wateja wao,” anasema.
Kuna wanaobashiri pia kwamba huenda baadhi ya klabu zikashuka kutokana na kukosekana kwa fedha kwenye mzunguko wao. Kihistoria, wamiliki hao wa klabu wamekuwa wakitoa fedha kama ruzuku kuongezea kwenye klabu kutoka kwenye mapato ya biashara zao.
“Sasa ikiwa biashara zao zenyewe zitaanza kuyumba, kitu kilichopata kutokea Bury mwaka jana, basi unaweza kuona kirahisi kwamba hali inaweza kujirudia zaidi kwa klabu nyingine ten ana tena, ikizingatiwa kwamba klabu hizi hutumia moja kwa moja fedha zote wanazotengeneza na bado wanategemea mishiko kutoka biashara za wamiliki,” anasema mtaalamu Maguire.
Lakini anasema jambo moja zuri lingeweza kufanywa, kwa EPL kutoa ushirikiano kwa klabu za ligi ndogo kutoka kwenye utajiri wake mkubwa ilio nao. Kwenye akaunti za karibuni kabisa za EPL, walikuwa na fedha taslimu zaidi ya pauni bilioni 1.5 zikiwa zimekaa tu kwenye hesabu zao.
Ni kweli kwamba ipo mipango ya kugawa fedha hizo kwa wanachama wake, lakini EPL wanaweza kusea kwamba basi wafanye kitendo cha wema na imani njema kwa familia ya soka na kutoa walau £250,000 kwa kila klabu kwenye League One na League Two. Hapo wangekuwa wamegharimika pauni milioni 12 tu na kuwaokoa klabu katika muwambo waliomo.
EPL wanaweza kufanya hivyo kama zawadi tu lakini ikiwa haiwezekani basi wanaweza kutoa kama mkopo usiokuwa na riba, kutokana na mazingira magumua ambayo klabu ndogo zinapitioa sasa hivi kwa sababu ya janga la virusi vya corona. Hiyo ingekuwa kuonesha upendo na mshikamano lakini pia uongozi bora katika familia ya soka.
Tatizo jingine la kifedha ni kwenye ubashiri wa matokeo, ambapo watu wengi walishajitumbukiza humo, wakitengeneza fedha na wengine wakipoteza fedha iwapo timu walizobashiri kushinda hazifanyi hivyo. Hawa sasa wanajielekeza kwenye mambo mengine wakati mechi zikiwa zimeahirishwa kwa wingi kiasi hiki na virusi vikizidi kuwa tishio na kusambaa zaidi katika nchi mbalimbali.
Katika muda mfupi tumeweza kuona maduka binafsi ya ubashiri wa matokeo yakifungwa kwa sababu soka imesitishwa, lakini pia kwa sababu baadhi ya watu wameamua kujitenga peke peke kama njia ya kuepuka kuambukizwa ugonjwa huu mbaya.
Mbali na soka na ubashiri, kuna biashara nyingine nyingi zinazoendeshwa mgongoni mwa soka, nazo zimepata pigo kubwa na walio wake kuanza kuathirika kiuchumi kutokana na kuahirishwa kwa mechi za soka.
Athari pia zitakuwapo kwenye masuala ya sekta ya utalii lakini pia mauzo ya vifaa vya michezo na jezi za timu pendwa. Ni suala mtambuka linalosogea na kugusa pia masuala ya hoteli, kwa sababu wachezaji wengi wapo kivyao majumbani mwao. Hapo hujazungumzia usafiri na huduma nyingine mbalimbali.
Chukulia mfano wa Liverpool wanapocheza nyumbani pale Anfield – wakiwa na washabiki maelfu kwa maelfu. Wapo wanaosafiri na kuamua kulala hotelini kuanzia Ijumaa hadi Jumapili kwa ajili ya kushuhudia timu yao ikicheza kuelekea kuchukua ubingwa, lakini sasa hakuna kucheza tena; hoteli husika zinakuwa tupu. Kuna watu wanapoteza kazi, hasa wale waliokuwa wakifanya kama vibarua kwa maana ya kazi ya muda.
Kutokana na sintofahamu kwenye EPL na kwamba lini michuano itamalizika, au ikiwa muda ukimalizika kwa kalenda basi watachukulia bingwa aliye juu na timu za chini kushushwa daraja. Wengine wanasema kwamba vigezo na masharti hayatakuwa yamezingatiwa na kutekelezwa hivyo kuwapo uwezekano wa EPL kuburuzwa mahakamani. Kwa ujumla hadi sasa klabu na wadau wamepoteza au kukosa fedha.