Hatimaye baada ya safari ngumu yenye milima na mabonde, timu ya taifa ya soka ya England imefuzu kucheza Kombe la Dunia Brazil 2014.
England walipata ushindi muhimu wa mabao 2-0 dhidi ya Poland usiku wa kuamkia Jumatano hii katika Uwanja wa Wembley.
Alikuwa mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney na kiungo mkabaji wa Liverpool, Steven Gerrard ambaye pia ni nahodha wa timu zote hizo waliofunga mabao hayo.
Kocha Roy Hodgson alionesha furaha ya pekee na benchi lake la ufundi, baada ya ushindi huo kutokana na kupondwa awali na kuwa na hofu ya kutofuzu au kutupwa kwenye hatua za mchujo.
England walizihitaji pointi hizo tatu katika mechi ya mwisho kwenye kundi H hasa baada ya Ukraine kuwafyatua San Marino kwa mabao 8-0.
Hata hivyo Poland hawakuwa rahisi kuwashinda, kwani walianza kwa mashambulizi kabla ya Rooney kuvunja kizingiti chao kama alivyofanya dhidi ya Montenegro Ijumaa iliyopita.
Washabiki karibu 18,000 walisafiri kutoka Poland kuwashangilia vijana wao Wembley na nusura Robert Lewandowiski awalize Waingereza.
Washabiki wa England watakamilisha furaha yao kwa kwenda Brazil, ambapo tayari watu 97,000 wameshaomba tiketi kwa ajili ya kwenda kushuhudia mechi mbalimbali za England.
Timu nyingine zilizofuzu kwa michuano hiyo ni wenyeji Brazil, Australia, Japan, Iran, Korea Kusini, Ubelgiji, Italia, Urusi, Uswisi, Bosnia-Hercegovina, Ujerumani, Uholanzi, Hispania, Costa Rica, Marekani, Argentina na Colombia.
Katika matokeo mengine, Ubelgiji na Wales walitoka sare ya 1-1; Scotland wakawafunga Croatia 2-0; Jamhuri ya Ireland wakawafunga Kazakhstan 3-1 na Israel wakaenda sare ya 1-1 na Ireland Kaskazini.
Serbia waliwadonoa Macedonia 5-1; Bulgaria wakalala 0-1 kwa Jamhuri ya Czech; Denmark wakawabomoa Malta 6-1, Italia wakaenda sare ya 2-2 na Armenia; Visiwa vya Faroe wakalala 0-3 kwa Austria, Sweden nao wakapoteza kwa 3-5 mbele ya Ujerumani na Hungaria wakawashinda Andorra 2-0.
Comments
Loading…