Real Madrid wawapiga Barca
Barcelona na washabiki wao hawakuamini macho wala masikio yao usiku wa
kuamkia Jumapili hii, baada ya kuchapwa 2-1 na Real Madrid.
Ilikuwa siku muhimu kwa Barcelona kwenye mechi hii ya La Liga, kwani
kwanza walikuwa uwanja wa nyumbani, lakini pili ilikuwa ya buriani kwa
shujaa wao, hayati Johan Cruyf.
Uwanja wa Camp Nou ulipambwa kwa maneno ya kumsifu na kumuaga Cruyf
aliyecheza hapo, akiwa mmoja wa wachezaji walioasisi ‘Total Footbal.
Hata hivyo hali ya hewa ‘ilichafuliwa’ na Cristiano Ronaldo na Karim
Benzema waliofunga mabao ya wageni.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Madrid walimaliza mechi wakiwa watu 10 tu,
baada ya Sergio Ramos kupewa kadi ya pili ya njano na hivyo kuwa
nyekundu, kutokana na kumpiga kiwiko Luis Suarez. Kadi ya kwanza ya
njano ni kumchezea vibaya beki Dani Alves.
Ilikuwa siku ya furaha kubwa kwa kocha Zinedine Zidane aliyepata
ushindi wa kwanza katika El Clasico tangu achukue mikoba hiyo kutoka
kwa Rafa Benitez.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika kwa suluhu, alikuwa ni Gerald
Pique aliyefungua mambo kwa kupiga kichwa cha nguvu na kufunga katika
dakika ya 57.
Hata hivyo, dakika tatu tu baadaye, Benzema alisawazisha. Bao la
Gareth Bale lilikataliwa baada ya mwamuzi kudai kwamba alikuwa
amemsukuma Jordi Alba.
Machungu ya Madrid yalizidi pale Ramos alipotolewa nje dakika ya 82
lakini dakika tano kabla ya kipenga cha mwisho, Ronaldo alifunga bao
akiwa karibu kabisa na lango na kuwahakikishia Madrid ushindi. Hili ni
pigo lisilosahaulika kwa Barcelona, kwani wamevunjiwa rekodi yao ya
kwenda mechi 39 bila kufungwa.
Mapacha watatu kwenye ushambuliaji – Lionel Messi, Neymar na Suarez
hawakumudu kuwavuruga Madrid na ndoto za Messi kufikisha mabao 500
katika mechi hiyo zilionekana kuwa za alinacha.