Ebola inaendelea kufukuta.
Mbali na zaidi marehemu 5,000 nchini Liberia, Guinea na Sierra Leone, shirika la uganga la kujitolea “Medicines Sans Frontieres” lilimekiri wiki hii kwamba hatua za kuukabili ugonjwa zinazidiwa nguvu. Msemaji wa MSF, Andre Heller-Perache alililiambia gazeti la “Guardian”, Uingereza kuwa bado waganga wa kujitolea wanahitajika.
Ingawa takwimu zinaonyesha wagonjwa wamepungua kidogo Liberia, bado hali si nzuri hata kidogo, Bwana Heller-Perache alisisitiza. MSF, imekuwa mstari wa mbele kusaidia maeneo yenye Ebola. Hali ni ya utata kiasi ambacho Ebola imeanza kuathiri starehe na michezo.
Shindano muhimu la kila miaka miwili la kombe la Afrika limekuwa mwathirika mkubwa baada ya Morocco kutimuliwa na Shirikisho la mpira Afrika (CAF).
Hii ina maana wachezaji maarufu wa Morocco wanaocheza ligi ya Uingereza, Marouane Chamakh(Crystal Palace), Adel Taarabt (QPR) na Oussama Assadi (Stoke), hawatachangamsha kadamnasi, mwakani.
Uamuzi wa kuitimua Morocco umepitishwa baada ya nchi hiyo kupendekeza mashindano yaahirishwe hadi mwezi Juni 2015 au Januari 2016. Kufuatana na shirika la Afya duniani (WHO), Morocco haina hata mgonjwa mmoja wa Ebola.
Morocco ilieleza hofu zake kushirikisha wachezaji na watazamaji mbalimbali nchini humo, hasa kutoka Afrika Magharibi, mwakani na kusababisha kuenea maradhi. Michuano hiyo inatazamiwa kuanza tarehe 17 Januari hadi 8 Februari, 2015.
“Uamuzi wetu umepewa motisha na tishio la kirusi hiki litakaloathiri afya ya Waafrika wenzetu,” Waziri wa Michezo wa Morocco, Mohamed Ouzzine alisema katika taarifa.
Morocco si nchi ya kwanza kuonesha kutopenda kushirikisha mchezo huu kutokana na Ebola. Mwezi Agosti, Seychelles ilikataa kucheza na Sierra Leone kwa woga wa Ebola. Nahodha wa Sierra Leone , Kei Kamara, baadaye aliiambia BBC kuenea kwa maradhi haya ni kama sinema ya kubuni ya “mazuzu wa kisayansi.”
Mara ya mwisho Morocco kuwa mwenyeji wa michuano ilikuwa 1988. Morocco ilitwaa kombe la bara kwa kuichapa Cameroon bao moja kwa bila.
Morocco ilikuwa taifa la kwanza la Kiafrika na Kiarabu kushiriki mara ya pili, Mexico1986. Morocco inayojulikana kwa jina Al Maghrib (Magharibi), ina wakazi milioni 33 na mji wake mkuu ni Rabat.
Hadi tukiingia mitamboni leo alfajiri, shirika la CAF lilikuwa likiwaza na kuwazua wapi mashindano yafanyike. Shirika halitazamii hata kidogo kuahirisha mashindano haya kwa hofu ya kupoteza mamilioni ya fedha.
Kati ya nchi zilizowekwa mstari wa mbele kuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka 2015 ni Algeria , Gabon, Nigeria, Misri na Angola. Hata hivyo kila nchi
ina kasoro yake. Algeria iliyokuwa mwenyeji mwaka 1990 inachunguzwa zaidi kutokana na namna watazamaji wake walivyo wakorofi. Mwezi Agosti, mchezaji wa Cameroon, Albert Ebosse Bodjongo alifariki baada ya mtazamaji mmoja kumrushia kitu kichwani wakati wa mechi baina ya JS Kabylie na USM Alger.
Wenyeji wa mwaka 2000 na washindi wa kombe mwaka jana, Nigeria, wana tatizo la ugaidi wa Boko Haram.
Misri ilikaribisha washindani mwaka 2006 na imeshinda kombe mara sita. Lakini sasa hivi machafuko ya kisiasa ni makali sana humo. Nchi pekee iliyotulia ni Gabon, mwenyeji mwaka 2012. Hakuna baya lililosemwa hadi sasa.
Ingawa Morocco imekataliwa bado itakuwa mwenyeji wa michuano ya klabu za FIFA ya dunia mwezi ujao kwa siku kumi. Kati ya timu kubwa zinazotazamiwa kushiriki ni Real Madrid.
Comments
Loading…