*Giroud aumia, hatima yake shakani
*Lampard aachia ngazi timu ya taifa
* MK DONS 4 MAN UTD 0
Manchester United wamekubali kutoa kitita cha pauni milioni 59.7 kumsajili winga wa Real Madrid, Angel Di Maria.
Raia huyo wa Argentina alitua Manchester Jumanne hii asubuhi kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya na baada ya hapo kuendelea kukamilisha mipango ya usajili, ambapo United watakuwa wametumia pauni milioni 132 katika msimu huu wa kiangazi.
Ada hiyo imevunja rekodi ya uhamisho katika historia ya wachezaji kusajiliwa Uingereza, ambapo aliyekuwa akiishikilia kwa kusajiliwa kwa kiasi kikubwa zaidi ni Fernando Torres wa Chelsea ambao waliwalipa Liverpool pauni milioni 50 mwaka 2011.
Walikuwa ni United pia waliovunja rekodi ya Uingereza mwaka 2002 walipomsajili Rio Ferdinand wka pauni milioni 29.1 kutoka Leeds. Man U tayari wamemsajili beki wa kushoto, Luke Shaw, kiungo Ander Herrera Marcos Rojo kwa jumla ya pauni milioni 72.
Real Madrid wamempa ruhusa ya kuondoka kwa sababu wanajua Di Maria hangekubali kuhuisha mkataba wake kwa malipo ya sasa, ambapo angekuwa chini sana yakilinganishwa na ya Cristiano Ronaldo na Gareth Bale.
Di Maria alijiunga Real Madrid 2010 akitoka Benfica kwa ada ya uhamisho ya £36m. Rais wa zamani wa Real Madrid, Ramon Calderon ameeleza kusikitishwa kwake na taarifa za kuondoka kwa Di Maria, akisema kwamba kwa kawaida klabu zenye wachezaji wazuri hazipendi kuwaachia.
GIROUD HUENDA AKAWA NJE MIEZI MITATU
Arsenal wameingia katika hali ngumu kimajeruhi mapema msimu huu, ambapo Olivier Giroud ameumia enka na anadhaniwa atakuwa nje kwa karibu miezi mitatu.
Alifanyiwa vipimo mara mbili, lakini kutokana na uvimbe mkubwa, haikuweza kuelezwa moja kwa moja ikiwa alikuwa amevunjika, na kama ndivyo atakuwa nje kwa muda mrefu, na lazima watafute mshambuliaji mwingine wa kati.
Mfaransa huyo atakosa mechi ya Jumatano hii ya mkondo wa pili kufuzu kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Besiktas katika dimba la Emirates. Mechi ya kwanza nchini Uturuki ilimalizika kwa sare tasa.
Kuumia huko kunakuja wakati kuna habari za Lukas Podolski kutaka kuhama kwenda ama Juventus nchini Italia au Wolfsburg, kwao, Ujerumani. Arsenal wanadaiwa kufikiria kumsajili Danny Welbeck wa Manchester United au Loic Remy wa Queens Park Rangers.
Arsenal wapo katika wakati mgumu, ambapo kwenye mechi ya UCL watamkosa Aaron Ramsey anayetisha kwa mchezo mzuri kwenye kiungo na kufunga mabao, kwani ana kadi mbili za njano, hivyo atakosa mechi moja.
Alexis Sanchez aliyesajiliwa msimu huu kutoka Barcelona kwa pauni milioni 35 bado hajaonesha cheche zake, na kwenye mechi dhidi ya Everton alitolewa baada ya kipindi cha kwanza, nafasi yake ikachukuliwa na Giroud aliyefufua uhai kwenye ushambuliaji.
Wengine wanaoweza kucheza kwenye nafasi hiyo ya ushambuliaji wa kati ni chipukizi Yaya Sanogo aliyepona majeraha yake, lakini pia Joel Campbell anaweza kucheza. Nahodha, Mikel Arteta atakuwa nje kutokana na kuumia.
LAMPARD KWA HERI THREE LIONS
Mchezaji wa New York City aliye kwa mkopo Manchester City, Frank Lampard ametangaza kustaafu kuchezea Timu ya Taifa ya England, Three Lions, baada ya kuitumikia katika mechi 106.
Kiungo huyo aliyeachwa na Chelsea baada ya mkataba wake kumalizika majira haya ya joto, alicheza mechi yake ya mwisho kwenye fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Costa Rica, ambapo walitoka 0-0.
Lampard (26) alianza kucheza 1999 na anamfuata Steven Gerrard wa Liverpool aliyetangaza majuzi kustaafu kuichezea timu ya taifa inayofundishwa na Roy Hodgson.
“Imekuwa vigumu sana kwangu kufikia uamuzi huu, ndiyo maana nimechukua muda mrefu hivi tangu baada ya fainali za Kombe la Dunia,” akasema Lampard ambaye pia amepata kuwa nahodha msaidizi.
Comments
Loading…