*Wanaungana na Cardiff na Hull EPL
*Benitez ateuliwa kocha mkuu Napoli
Hatimaye kitendawili cha timu zitakazocheza Ligi Kuu ya England (EPL) msimu ujao kimeteguliwa katika uwanja wa Wembley, baada ya Crystal Palace kutwaa nafasi ya tatu na ya mwisho katika mchezo mkali dhidi ya Watford.
Palace wanaungana na klabu nyingine mbili zilizokuwa nayo ngazi ya pili ya ligi – Championship – Cardiff City na Hull City kuingia kwenye ligi kubwa zaidi nchini Uingereza na maarufu zaidi ya zote duniani, ambapo hatua hiyo inathamanishwa na pauni milioni 120, kwa uchache.
Palace walikwenda hadi muda wa ziada kupata ushindi wao kwa mkwaju mmoja wa penati, baada ya Wilfred Zaha kuchezewa vibaya kwenye eneo la penati, ambapo mkongwe Kevin Philips alikwamisha wavuni shuti kali, na kumwacha nahodha wa Watford na kipa wa zamani wa Arsenal, Manuel Almunia akiukosa, japo aliuendea juu kona ya kulia.
Zaha anaondoka kwenda Manchester United msimu ujao, na amechangia kwa kiasi kikubwa kuwapandisha daraja Palace, wakati Philips naye anasema anapumzika soka, na atafikiria baadaye kipi cha kufanya, kama kucheza tena au kuwa kocha, maana sasa ana umri wa miaka 39.
Kocha Ian Holloway alionesha furaha isiyo ya kawaida kwa ushindi huo, akionekana mtu muhimu aliyeifufua, baada ya kupoteza makali yake, na miaka michache iliyopita ilikaribia kusambaratika na kushuka daraja 2009/10, baada ya kufilisika.
Kocha wa Watford, mchezaji mahiri wa zamani, Giafranco Zolla alijawa masikitiko, pamoja na mchezaji Marco Casseti aliyesababisha penati kwa rafu ambayo haikuwa ya lazima, na laiti wangeendeleza kukaba vyema, mchezo ungeenda hadi kwenye matuta. Watford nusura wasawazishe dakika za lala salama, lakini mpira wa kichwa wa Joel Ward uliokolewa kwenye mstari na Fernando Forestieri.
Palace wanaweka rekodi kuwa klabu ya kwanza kupanda EPL kwa mara tano, na safari hii Holloway anasema watagangalama na kubaki, si kama mara zilizopita. Mara ya mwisho walishuka daraja mwaka 2005.
RAFA BENITEZ KAMA MFALME ITALIA
Kocha wa Muda wa Chelsea, Rafael Benitez Maudes ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa Napoli ya Italia. Rafa Benitez (53) alikuwa akisubiri kazi mpya, kwani aliyokuwa nayo ilikuwa ya muda hadi mwisho wa msimu huu, na huko Italia anachukua nafasi ya Walter Mazzurri aliyefukuzwa na kujiunga na wapinzani wa jadi wa Napoli kwenye Serie A, Inter Milan.
Rais wa Napoli iliyoshika nafasi ya pili msimu huu, Aurelio De Laurentiis amemwelezea Benitez kuwa ni mtu maarufu mwenye uzoefu wa kimataifa na kwamba ni kiongozi mzuri ambaye atawawezesha Napoli kutwa mataji msimu ujao.
Rais huyo hivi majuzi alikuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa kwenye hafla kubwa, akasema kwamba amepata zawadi ya pekee kwa siku hiyo, na kwamba ilikuwa kocha nguli, Benitez, japokuwa baadaye alikanusha kumtaja jina, akisema bado ameajiriwa Chelsea na anapenda kufuata sheria na kanuni.
Benitez aliyepata umaarufu zaidi kwa miaka mingi aliyowaongoza Liverpool, anamaliza kazi Chelsea kwa kuwapatia Kombe la Europa na nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, hivyo kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani.
Benitez pia aliwafikisha Chelsea kwenye Kombe la Dunia la Klabu la Fifa walikofungwa na Corithians ya Brazil na kabla ya hapo aliwaongoza Valencia ya Hispania kutwaa taji la La Liga (2001-02, 2003-04); Kombe la Uefa (2003-04); Liverpool Kombe la FA (2005-06); Ngao ya Jamii (2006); Kombe la Ulaya (2004-05); Uefa Super Cup (2005). Pia aliwaongoza Inter Milan kutwaa Supercoppa Italiana (2010) na Kombe la Dunia la Klabu la Fifa mwaka 2010.
Pamoja na mafanikio hayo, hakuwa akipendwa na washabiki wa Chelsea, waliozoea kumzomea na kumshikia mabango ya kumtaka aondoke, wakionesha wazi kuchukizwa na jinsi mtangulizi wake, Roberto Di Matteo alivyofukuzwa kazi. Inatarajiwa kwamba Jose Mourinho atajiunga Chelsea baada ya kuaga Real Madrid rasmi.
Comments
Loading…