Alosto ya kukosa kushuhudia mechi za ligi mbalimbali duniani ni kubwa kuliko kula chakula unachokipenda zaidi hasa ubwabwa, kwa wanamichezo watakuwa wanaelewa namna tunavyotaabika kukosa mikikimikiki ya ligi.
Kwa kawaida imezoeleka ikifika mwezi Mei hadi Juni ligi zote zinakuwa zimemalizika na tunakaa miezi miwili kisha tunarudi mzigoni katika maisha yetu ya kawaida ya michezo.
Hapa Afrika Mahsariki mashabiki wengi wa Manchester United ikifuatiwa na Arsenal huku Liverpool wakiwa wamejikusanya tena Chelsea nayo ipo humo basi huwa kuna utani sana kila wiki kutokana na matokeo ya timu hizo.
Maisha ya kutaniana baina ya timu hizo yamekuwa na afya kubwa kwa wanamichezo na wengi wamekikosa kwa miezi miwili sasa kutokana na ugonjwa huo.
Katika miezi hiyo miwili bado kunakuwa na mechi za kirafiki kwa timu mbalimbali maarufu kama ‘Club Friendly match’ bado macho ya watu wa michezo yanazidi kutizama michezo na mechi mbalimbali.
Sasa maambukizi ya virusi vinavyosabisha Korona(COVID-19) imekuja kuharibu mipango mbalimbali ya wanamichezo hasa wachambuzi wa soka katika kupiga mkwanja.
Kwa Afrika kukosekana kwa kuendelea kwa ligi kubwa kumeathiri sana maisha ya wachambuzi ‘Pundit’ katika vituo mbalimbali vya Televisheni(TV).
Baadhi ya wachambuzi kutoka Tanzania na sehemu mbalimbali za Afrika walikuwa wanaenda Afrika Kusini kutangaza mechi za ligi pendwa na wengine kuchambua huwa wanapata pesa nyingi sana, hii yote kutokana na utajiri wa matangazo yanayotokana na michezo kitu kimoja kinachoitwa Korona kimekuja kumwaga mboga za wachambuzi na watangazaji.
Kwa Tanzania imeathiri sana kwa mifano halisi inaonekana karibuni vituo vyote vina vipindi vya michezo na kuna baadhi ya wachambuzi hualikwa katika vituo hivyo japo malipo yao sio mazuri sana lakini yalikuwa yanasogeza maisha yao kwa wahusika.
Ilivyokuja Korona ilifanya kila kituo kuogopa kupokea wageni kwa kujihami kwa kuenea maambuzi ya virusi, hiyo ni athari moja wapo ya ugonjwa huo.
Mfano huu unafanana kabisa na nchi nyingi za Kiafrika mara nyingi zinafana kwa kila matukio yao, inatokana na mfumo wa michezo barani humo.
Kuna wale wa kupiga pesa kupitia tiketi za uwanjani nao wamekosa ulaji huu kutokana na janga hili, hii inategemea sana na dua pamoja na sala kuomba ugonjwa huu uishe , sio tu Tanzania bali duniani kote inaweza kurudisha maisha ya watu kwenda vizuri.
Huko duniani vituo kama Sky Sports, BBC Sports na vituo vingine navyo vimesimamisha shughuli hii kwa kupisha ugonjwa wa Korona.
Walio wengi hivi sasa kwa nchi za Ulaya wanafanyia uchambuzi wakiwa kwao, hii pia inawapa wakati mgumu kwa wachambuzi wa soka.
Kwa wale waliokuwa wanafanya kazi viwanjani nako hakuliki sasa maana hakuna kinachoendelea.
Kwa wale wa vibanda umiza nao wanakosa pesa kwani watazamaji walikuwa wanajazana kuangalia ligi mbali mbali duniani.
Moja ya wamiliki wa Kibanda umiza maarufu sana hapa Kinondoni Moscow Dar es Salaam, Uwesu Ngwabi ameichukulia Korona kama changamoto nyingine ila amekiri kukosa fedha nyingi sana kupitia kuonesha ligi mbalimbali.
Amesema kuwa kila wiki alikuwa na uhakika wa kuingiza laki mbili na hamsini kwa kuonesha mechi mbalimbali, tangu uingie ugonjwa huo hajapat kabisa kiasi hiko kwa wiki.
“Huu ugonjwa noma sana, umeniharibia kuongeza kipato changu, kwa miezi hii miwili nimekosa laki mbili na nusu kila wiki kuonesha ligi mbalimbali,”alisema.
Aliweka bayana kuwa ligi kuu England maarufu kama ‘EPL’ ndio sehemu kubwa inayomuingizia kipato huku mechi za ligi kuu Tanzania bara inapocheza Yanga au Simba watu wanajaa sana na ndio sehemu ya kupiga pesa.
“Ligi kuu England inanipa fedha nyingi sana hasa washabiki wengi wanapenda timu za huko kuliko ligi nyingine, kwa hapa nyumbani Yanga na Simba inapocheza na timu yoyote nako natengeneza mpunga mwingi(fedha) sana,”aliongeza.
Mchambuzi wa michezo anayekuja kwa kasi nchini Tanzania Yahya Njenge yeye ameitazama korona katika sekta hiyo kwa jicho la pili.
Amekubali kuwa wachambuzi wengi wanategemea michezo kuweza kualikwa na kutengeneza kipato hivyo kiuchumi imeathiri sana,” Alisema Njenge.
Pia amesema vipindi vyenyewe vya michezo vimepooza sana kwa kuwa hakuna matukio ya maana ya kuyachambua hivyo vipindi vingi vinakosa ladha vinakuwa katika mlengo wa kuangalia historia za wachezaji wa zamani au takwimu zilizopita.
“Vipindi vyenyewe vimepooza sana kwakuwa hakuna maudhui na matukio yaliyo bora ya kuchambua, kwa aina hiyo pia inawaboa wasikilizaji wetu, vipindi vingi vimepooza sana,”aliongeza.
Hata hivyo tayari ligi mbalimbali zimeanza kurejea, Burundi imekuwa nchi ya kwanza kurejesha ligi wakati huo Ujerumani nao wiki iliyopita wamerudisha ligi, Tanzania Juni Mosi inarudi hivyo maisha yataendelea kama ilivyokuwa zamani, michongo itarudi kama ilivyokuwa.
Janga hili kama ilivyo majanga mengine yaliyowahi kupita, mfano Surua,Pepopunda na Ukwimi na kwa uwezo wa Mugu litapita maisha mengine yataendelea.