Viongozi wengi wa soka nchini Tanzania hulenga kujinufaisha binafsi badala ya kuendeleza timu ili zijitegemee na kufanikiwa.
Hutumia nafasi wanazopata kwa namna tofauti kuchumia matumbo yao, iwe kwenye klabu, timu za taifa na vyama.
Ni bahati mbaya sana pia kwamba watu wakweli hupigwa vita kwenye nafasi hizo pindi wanapobainika. Kwa jinsi hii ni vigumu kufikia malengo yanayotakiwa na umma wa wapenda soka.
Coastal Union ya Tanga wamemaliza Ligi Kuu ya Soka Tanzania wakiwa nafasi ya tisa; mbaya zaidi ni kwamba wamefungwa mechi nyingi (tisa) kuliko zile walizoshinda ambazo ni sita tu.
Kabla ya kuanza kuanzisha malumbano kati ya Mfadhili wa timu, Nassor Binslum na Mwenyekiti Ahmed Aurora kuhusu madai ya fedha, walitakiwa kuanza na hili la mwenendo mbaya wa timu yao kwenye ligi iliyomalizika hivi majuzi.
Coastal Union ni moja ya timu nne zilizokuwa zikipewa nafasi ya kufanya vizuri na hata kutwaa ubingwa wa msimu huu.
Nyingine ni Simba, Yanga na Azam. Hakuna aliyewaza kuihusisha Mbeya City na ubingwa au hata kuwa nafasi nne za juu, pengine kutokana na ugeni wao kwenye ligi.
Coastal Union walipewa nafasi kutokana na usajili mzuri walioufanya, maandalizi yao ya kambi na safari ya nchini Oman, lakini kubwa zaidi ni jinsi wanavyoungwa mkono na wakazi wa jijini Tanga.
Kikosi cha timu hiyo kilikuwa kimekamilika karibu kwenye kila idara kwa sababu kilisheheni wachezaji wengi wenye ubora, uzoefu na pia kilikuwa na vijana waliotarajiwa kuipigania timu hiyo.
Nilifuatilia mechi kadhaa za timu hiyo na kiukweli nyakati nyingi timu ilishindwa kupata matokeo mazuri kutokana na kutojituma kwa baadhi ya wachezaji wao.
Hakuna hata mtu anayelitazama hilo na badala yake, picha limegeukia kwenye kupishana kauli kwa Binslum na Aaurora!
Ukimfuatilia vyema Binslum utaona kwamba kinachomtesa sana ni mapenzi yake ya dhati kwa timu hiyo.
Kwa Aurora, kupitia vyombo mbalimbali vya habari nimegundua ia kwamba anatatizwa na jinsi anavyolenga kuisaidia timu hiyo ‘kirafiki zaidi’ kuliko kibiashara kama soka la sasa linavyohitaji. Wote wawili wamenaswa hapo.
Tayari kuna taarifa kuwa viongozi wa Coastal Union wamebweteka kwa kuona kuna Sh milioni 100 za udhamini wa Azam kwa ajili ya kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mechi za Ligi Kuu na kupanda kwa fedha za mdhamini wa ligi – Vodacom.
Huko kumeanza kuwatia jeuri na kuandaa mkakati wa kuwaondoa watu wote wanaowabana ili wapate nafasi ya kuzipiga fedha hizo.
Kwa kufanya hivyo, haitakuwa kumkomoa Binsum wala Aurora bali ni kutowatendea haki wapenzi na wanachama wote wa Coastal Union.
Wananchi wa Tanga wanahitaji kuona timu yao ikirejea kwenye ubora na kurejesha heshima ambayo waliwahi kuipata mwishoni mwa miaka ya 1980 kwa kutwaa ubingwa wa Tanzania.
Golikipa Shaaban Kado, kiungo mshambuliaji Haruna Moshi na beki kisiki Juma Nyosso wanaelezwa kuwa wamemaliza mikataba yao ya kuitumikia klabu hiyo.
Huu ni muda mwafaka wa kupitia ripoti ya mwalimu na kubaini nani anatakiwa kubaki na yupi anatakiwa kuondoka ili kuijenga timu imara kwa ajili ya msimu ujao.
Kumekuwa na malalamiko pia kuhusu namna uongozi wa timu hiyo unavyozuia kijanja kutoa fomu za uanachama huku ikisemekana wanaogopa vijana mbao kama watapata kadi za uanachama watakuja baadae kuwaondoa madarakani.
Hii si haki na kwa taarifa tu hakuna marefu yasiyokuwa na ncha.
Binslum na Aurora wanatakiwa kumaliza tofauti zao na kuungana pamoja kwenye njia kuu ya kuiletea mafanikio timu yao.
Sioni kama kuna sababu ya msingi kwa Binslum kuihama timu hiyo au kusitisha misaada kwa sababu ni timu anayoipenda kwa dhati ya moyo wake; wafanye tu makubaliano ambayo ni rasmi ili kuondoa mgongano.
Comments
Loading…