Ligi Kuu ya England (EPL) iliyoingia mechi za 30 kwa timu nyingi imewaacha Chelsea katika nafasi nzuri, wakiwa kileleni kwa pointi zao 67 dhidi ya 61 za wanaowafuata, huku wakiwa na mechi moja mkononi.
Mwishoni mwa wiki vijana hao wa Jose Mourinho walipata ushindi mwembamba dhidi ya Hull, hivyo kufanya ngoma kuwa ngumu kwa wanaowania nafasi nyingine tatu ili kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Pengine inaweza kuwa hali ngumu zaidi kwa Liverpool waliokubali kupigwa na Manchester United, huku nahodha wao, Steven Gerrard akitolewa nje kwa kadi nyekundu.
Mbaya zaidi ni kwamba Liverpool watakutana na Arsenal kwenye mechi ijayo huku beki wake, Martin Skrtel naye akishitakiwa kwa kosa la kumkanyaga makusudi kipa wa United, David de Gea na kuwa na uwezekano wa kuadhibiwa.
Hayo yakijiri, wapambanaji wengine – Arsenal, Southampton na Tottenham Hotspur walifanya vyema, hivyo kufanya ushindani mkali. Man City wanashika nafasi ya pili kwa pointi 61, wakifuatiwa na Arsenal wenye 60 na Man United wenye 59. Liverpool wana 54 na Southampton 53.
Kuna timu saba zinazoonekana kukimbizana hapa, na hatima ya yote itajulikana mwisho wa siku ya msimu huu, Mei 24.
Kama Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal alivyowasifu vijana wake kwa ushindi muhimu dhidi ya Liverpool, Arsenal wana mtihani kama huo wikiendi hii.
Timu zilizo hatarini kushuka daraja zimebaki kuwa Leicester wenye pointi 19 na uwiano wa mabao -21, QPR wenye pointi 22 na uwiano wa mabao -23 sawa na Burnley wenye uwiano hio lakini pointi 25.
Sunderland wanachungulia eneo hilo wakiwa na pointi 26 na tayari wamemfukuza kocha wao, Gus Poyet. Aston Villa waliomfukuza kocha Paul Lambert nao wana pointi 28 sawa na Hull.
Comments
Loading…