*Fabregas alambwa kadi nyekundu
West Bromwich Albion wametibua mwendelezo wa sherehe za ubingwa wa Chelsea kwa kuwatandika mabao 3-0.
Katika hali ya kushangaza, kocha Jose Mourinho amelalamikia klabu nyingine kwa kichapo hicho, akidai hazikuonesha ushindani wa kutosha kwenye Ligi Kuu.
Aliyeanza kupeleka kilio kwa The Blues alikuwa ni mzaliwa wa Burundi, Saido Berahino ambaye pia alifunga la pili kwa penati kabla ya Chris Brunt kutia la tatu.
Penati hiyo ilitolewa baada ya nahodha wa Chelsea, John Terry kumwangusha Beraniho ndani ya eneo la penati.
Chelsea walimaliza mechi wakiwa 10 baada ya kiungo wake wa kimataifa wa Hispania, Cesc Fabregas kupewa kadi nyekundu.
Fabregas alipewa kadi nyekundu kwa kitendo chake cha kumpiga kwa mpira Brunt. Hiki kilikuwa kipigo cha tatu kwa Chelsea kwenye ligi msimu huu.
Kabla ya mechi hii Chelsea walikuwa wamekwenda michezo 16 bila kufungwa. Mshambuliaji wa kati wa Chelsea, Diego Costa naye alionekana kukwaruzana na beki wa kati wa West Brom, Gareth McAuley kiasi cha mwamuzi Mike Jones kuingilia kati kuwapatanisha.