Yametimia! Ndivyo unavyoweza kusema kwa vinara wa Ligi Kuu ya England, Chelsea kuambulia kichapo cha kwanza msimu huu.
Vijana wa Jose Mourinho walijizatiti kwa kushinda na mara chache kutika sare, lakini kwa gwaride la wachezaji wa Newcastle, wameishia kuwa mbendembende na ni leo baadhi ya wachezaji hao wamejua kufungwa Chelsea kunaumaje.
Newcastle wakicheza nyumbani na kwa kujiamini licha ya kuanza ligi kwa kusuasua msimu huu, walimaliza wakiwa wachezaji 10, kwani Steven Taylor alipewa kadi ya pili ya njano, na hivyo nyekundu kwa kumchezea vibaya André Schürrle katika dakika ya 80.
Mabao ya Newcastle yalitiwa kimiani na mchezaji aliyetamba misimu miwili iliyopita kabla ya kuwa doro, Papiss Cisse dakika za 57 na 78 wakati la kufutia machozi la Chelsea lilifungwa na Didier Drogba dakika ya 83.
Mourinho alisema kabla ya mechi hiyo kwamba alitarajia Newcastle wanaofunzwa na Alan Pardew wacheze gemu kali wanayokuwa nayo nyakati Fulani Fulani.
Kadhalika kichapo hicho kinakuja siku moja tu baada ya Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger kutamka kwamba Chelsea wanakamatika. Hadi kabla ya mechi hiyo walikuwa wanaongoza kwa pengo la pointi sita, wa pili wakiwa Manchester City.
Katika mechi hiyo, kipa wa Newcastle, Rob Elliot aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na kinda la miaka 21, Jak Alnwick. Hii ilikuwa mechi ya 15 msimu huu kwa Chelsea na Newcastle kwenye ligi kuu.
Cisse alifunga bao la kwanza baada ya beki Garry Cahil kushindwa kuzuia majalo iliyokuwa aimeingizwa kwenye eneo lao na Sammy Ameobi. Shuti la Eden Hazard baadaye lilimfikia Moussa Sissoko aliyekianzisha tena akampatia Cisse na kumfunga kipa Thibaut Courtois aliyekuwa hajafungwa kwenye ligi hii.