*Van Gaal akomaa haondoki Man United
*Cahil hofu Chelsea, Big Sam majina 60
Tetesi za nani atachukua nafasi ya Jose Mourinho klabuni Chelsea
zinazidi kutanuka.
Mpya mjini sasa ni kwamba wanamtaka kocha wa Timu ya Taifa ya Italia,
Antonio Conte, 46, anaweza kuchukua kiujumla mikoba ya The Special
One.
Baada ya kufukuzwa kazi kwa Mreno huyo, nafasi yake inashikiliwa kwa
muda, na kwa mafanikio kiasi, na Guus Hiddink aliyepata pia kuingia
Stamford Bridge kuwaokoa walipotaka kuzama.
Mtaalamu huyo anatarajiwa kuondoka mwishoni mwa msimu huku mmiliki
Roman Abramovich na viongozi wa Chelsea wakiumiza vichwa kupata bosi
wa kudumu.
Zimekuwapo tetesi pia kwamba Chelsea wanamfikiria kocha wa Tottenham
Hotspir, Maricio Pochettino anayefanya vyema White Hart Lane.
Lakini pia, zipo habari kuwa wanamfikiria kocha wa Bournemouth, Eddie Howe.
Hata hivyo, mwekezaji wa Bournemouth kutoka Marekani, Matt Hulsizer
anasema kwamba Howe, 38, haendi popote, akimaanisha hatamwachia.
Baadhi ya wadau wakidai Pep Guardiola ndiye chaguo tayari, japo
Manchester City wandaiwa wanamtaka akavae viatu vya Manuel Pellegrini
anayekosa uendelevu.
Hatima ya kocha wa Manchester United, Louis van Gaal inaendelea
kupamba vichwa vya magazeti mengi ya hapa, baadhi yakidai kwamba yupo
njiani kuondoka.
Hata hivyo, yeye mwenyewe anasema kwamba yupo Old Trafford na haendi
popote, ndiyo maana amekuwa akitafuta nyumba nyingine.
Anataka kuhakikisha anamaliza mkataba wake wa miaka mitatu aliosaini
hapo, na wakala wake alikuwa akimtafutia nyumba eneo la Cheshire.
Akizungumza kabla ya mechi ya Ijumaa hii dhidi ya Derby, Van Gaal
amesema kwamba akishindwa mechi hiyo anaweza ‘kufukuzwa kwa mara ya
nne’, akionesha kuwabeza waliosema kwamba amefikia kufukuzwa kazi mara
tatu.
Zimekuwapo habari pia kwamba Guardiola kuaga kwake Bayern Munich
mwishoni mwa msimu kunamaanisha anaingia United.
Pia Mourinho ameshatuma barua United akiomba apewe nafasi ya Mdachi
huyo anayedaiwa kushindwa kufikia mafanikio tarajiwa.
Kadhalika tetesi nyingine ni kwamba Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa Man
U, Ed Woodward na viongozi wenzake, wana wasiwasi katika kufanya
uamuzi hata akiondoka Van Gaal, kwani wasipompa nafasi hiyo kocha
msaidizi Ryan Giggs, na kwamba anaweza kukatisha miaka yake 18
aliyokaa Old Trafford kama mchezaji, kocha wa mpito na sasa kocha
msaidizi.
Manchester United wanamtaka mshambuliaji wa CSKA Moscow kutoka
Nigeria, Ahmed Musa, ambaye tayari anawaniwa na vinara wa Ligi Kuu ya
England, Leicester.
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp anafikiria kutoa pauni milioni 11 kwa
ajili ya kumnunua kiungo wa Udinese na raia wa Poland, Piotr
Zielinski, 21.
Mlinzi wa Chelsea, Gary Cahill, anayehofia kuikosa michuano ya Euro
2016, anatakiwa na klabu ya Italia ya Roma. Cahil ametupwa benchi na
kocha Hiddink kwa muda sasa.
Mchezaji huyo wa zamani wa Aston Villa na Bolton mwenye umri wa miaka
30 angewafaa Liverpool kuboresha ngome yao.
Mshambuliaji wa Barcelona, Neymar, 23, anasema angependa kucheza chini
ya kocha Pep Guardiola, hivyo kuacha maswali iwapo atasubiri aone
anakwenda wapi ndipo wakala wake aunganishe mambo.
West Bromwich Albion wanafanya mazungumzo na Queens Park Rangers (QPR)
kwa ajili ya kumpata kwa mkopo mchezaji wa zamani wa Spurs, Sandro.
Mlinzi wa New York Red Bulls, Matt Miazga, 20, alikuwa London Alhamisi
hii kwa ajili ya vipimo vya afya kabla ya kujiunga Chelsea.
Arsenal wamekataliwa ofa yao ya pili waliyopeleka Leicester kwa ajili
ya mlinzi wao mwenye umri wa miaka 19, Ben Chilwell.
Newcastle wanafikiria kuachana na mipango ya kumsajili mshambuliaji wa
West Brom, Saido Berahino na kutafuta mchezaji mbadala.
Magpies walikuwa tayari kutoa pauni zaidi ya milioni 20 kumpata
mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 lakini West Brom hawatoi
ushirikiano.
Newcastle wanatarajiwa kumfuata mshambuliaji wa Chelsea, Loic Remy,
29, aliyefunga mabao 14 katika mechi 26 za ligi kuu alipokuwa
Newcastle kwa mkopo msimu wa 2013/14.
West Ham na Norwich wanapigana vikumbo kumsajili mlinzi wa Inter
Milan, Davide Santon, 25.
Manchester United wanataka kumsajili kiungo Mreno wa Chelsea, Domingos
Quina, 16, aliyeingia akademia ya Stamford Bridge akiwa na umri wa
miaka 13.
Kocha wa Sunderland, Sam Allardyce amesema ana orodha ya majina ya
wachezaji 60, na kutoka humo atapata wa kusajili katika dirisha hili
dogo linalofungwa mapema Februari.
Katika hali ya kushangaza, kocha wa Crystal Palace, Alan Pardew tayari
ana wasiwasi kwamba mchezaji wake mpya, Emmanuel Adebayor, 31, anaweza
kuondoka bure mwishoni mwa msimu.
Adebayor amekuwa mtovu wa tabia lakini pia ameonekana kuathirika
kisaikolojia baada ya kukorofishana na familia yake – mama mzazi, kaka
na adada yake, akidai wamekuwa wakimloga ili ashuke kiwango alipokuwa
Spurs.