in , , ,

Chelsea wachanua tena

*Wawatandika Man United kwao
*Liverpool wawavimbia Everton

Baada ya ‘kuishi kwa matumaini’ kwa dakika 86 dimbani Old Trafford, Chelsea wameweka hai matumaini ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kuwaadhiri Manchester United kwa bao 1-0.
Chelsea wamechupa kutoka nafasi ya tano hadi ya tatu, wakiwashusha Arsenal kutoka hapo hadi ya nne, na ya tano wakichukua Tottenham Hotspurs. Awali ilidhaniwa mechi ingekuwa rahisi kwa Chelsea, kwa jinsi kocha Alex Ferguson alivyopangua kikiso chake, lakini dimbani haikuwa hivyo.
Golikipa namba moja, David Da Gea, Rio Ferdinand wala Michael Carrick ambao ni muhimu hawakucheza, hata Wayne Rooney aliingia baadaye, huku Robin van Persie akiwa kama hayupo uwanjani, isipokuwa kwa nyakati chache, lakini aliliona lango likiwa mbali mno.
Vijana wa Rafa Benitez, ambaye alipena mkono na Ferguson kabla na baada ya mechi, walijituma lakini ilibidi wasubiri hadi dakika ya 87, Phil Jones alipojifunga katika harakati za kuokoa mkwaju wa Juan Mata.
Beki Rafael wa United alipewa kadi nyekundu dakika za lala salama, baada ya kumchezea rafu David Luiz wa Chelsea, ambapo mara kadhaa mwamuzi Howard Webb alilalamikiwa ama kwa kupeta au kutoa adhabu. Rooney alilalamika kwa kutoadhibiwa Ramires aliyemkwatua.
Chelsea wana mechi nyingine muhimu Jumatano hii, dhidi ya Spurs, inayoweza kutoa mwelekeo zaidi wa timu zitakazoshika nafasi tatu za juu, ukiachilia mbali United ambao tayari ni mabingwa. Manchester City wanashika nafasi ya pili lakini bado wanahitaji pointi mbili kujihakikishia kucheza mashindano hayo makubwa ya Ulaya.
Wakati United wamebaki na pointi zao 85, City wanazo 72, Chelsea 68, Arsenal 67 na Spurs 65. Spurs na Chelsea wakicheza mechi ya Jumatano, watalingana na Arsenal kwa michezo waliyocheza, na baada ya hapo kila timu itakuwa imebakiwa na mechi mbili kumaliza ligi.
Liverpool, Everton Wakamiana na Kugawana Pointi
Katika mechi ya awali ya watani wa jadi wa Merseyside – Liverpool na Everton, hakuna aliyetoka mbabe, baada ya kugawana pointi, huku wakitunishiana misuli tangu mwanzo hadi mwisho.
Everton ambao wamepata kulalamikiwa na makocha, akiwamo wa Arsenal, Arsene Wenger kwa utumiaji wao wa miraba minne waliyo nayo dhidi ya wapinzani wao, walipata bao lililokataliwa na mwamuzi Michael Oliver.
Iwapo goli hilo lingeruhusiwa, Everton wangepata ushindi wa kwanza tangu 1999 uwanjani Anfield, lakini bao hilo lililotokana na kona ya Leighton Baines lilikataliwa kwa maelezo kwamba Victor Anichebe alimchezea vibaya kipa Pepe Reina. Anichebe alipinga na kuzawadiwa kadi ya njano.
Sare hiyo inawakatisha tamaa Everton kuweza kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, maana wameachwa pointi tano nyuma ya Spurs na pia pointi tano mbele ya mahasimu wao Liverpool.
Kabla ya mechi hiyo, nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard na kocha wa Everton, David Moyes walieleza kutoridhishwa kwao na jinsi klabu mbili hizo za Merseyside zimekuwa zikibaki nyuma mno ya wenzao wa Manchester.
Hata hivyo, Liverpool wanaonekana kuanza kujiimarisha, wakielekea kukamilisha msimu na kocha wao mpya, Brendan Rodgers, wakati Everton wanahitimisha wakiwa hawana uhakika kama Moyes atabaki nao, kwani alisema anasubiri kuona watamaliza nafasi gani. Mkataba wa kocha huyo aliyewatumikia kwa miaka 11 unamalizika majira haya ya kiangazi.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

*AZAM FC KUREJEA NYUMBANI KESHO*

Sunderland wapigana kiume