Arsenal wamekwenda suluhu na Liverpool kwenye mechi ya Ligi Kuu ya England (EPL) iliyofanyika kwenye dimba la Emirates, ambapo kipa wa kimataifa wa The Gunners, Petr Cech alithibitisha kwamba ni kifaa.
Kipa huyo aliyesajiliwa kiangazi hiki kutoka Chelsea alikuwa gumzo la mechi, ambapo hata kocha wa Liverpool alimkubali, akisema kwamba ndiye aliyekuwa mchezaji bora kwenye mechi hiyo ngumu.
Cech aliwapanga vyema mabeki wake, lakini walipoonesha udhaifu naye akiwa mtu wa mwisho alifanya kile ambacho kipa wa kiwango cha juu hufanya, akiokoa mabao mawili ya wazi, lakini pia mara nane akijituma kuhakikisha Liver hawatikisi nyavu za timu yake.
Arsenal walipomnunua Cech kwa karibu pauni milioni 10, wachambuzi walisema uwapo wake tu golini unawapa mabeki wake kujiamini na pia angeweza kusaidia timu kupata walau pointi 10 zaidi kuliko ambavyo hangekuwapo. Alianza vibaya mechi ya kwanza, kwani walifungwa 2-0 na West Ham.
Ulikuwa mchezo ambao Liverpool wameendeleza rekodi ya kutofungwa katika mechi tatu, wakiwa wameshinda mbili za mwanzo, lakini kulikuwa na umahiri langoni mwa wapinzani wao huku kukiwa na makosa kadhaa katika ukabaji, ambapo mabeki waandamizi wa Arsenal, Per Mertesacker na Laurent Koscielny hawakuwa uwanjani.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mabeki hao wawili wa kati kukosa mechi ya EPL kwa Arsenal tangu Aprili 2012 walipoikosa dhidi ya Wigan.
Liverpool walitawala kipindi cha kwanza lakini wakakutana na kigingi cha Cech, ambapo mshambuliaji wao mpya kutoka Aston Villa, Christian Benteke aliamini anafunga bao, lakini kama muujiza Cech akaokoa kabla ya kupangua tena kiki ya Philippe Coutinho.
Aaron Ramsey alifunga bao lakini mwamuzi, Michael Oliver akalikataa kwa madai kwamba alikuwa ameotea, uamuzi ambao haukumfurahisha kocha Arsene Wenger aliyesema kwamba Liverpool wamekuwa wakifaidika kwa uamuzi wa waamuzi.
Arsenal walijikusanya upya na kutawala kipindi cha pili, ambapo Alexis Sanchez alionesha kiwango katika mashambulizi, na moja ya mikwaju yake ukagonga mwamba huku kipa Simon Mignolet akifanya kazi ya ziada kumzuia mshambuliaji wa kati, Olivier Giroud kufunga.
Wenger alisema jana kwamba timu yake bado ni ya kawaida sana, na kwamba walifunga bao la kawaida lakini likakataliwa bali anaamini hana cha kufanya kubadili matokeo. Akasema upende usipende ni kweli kwamba mwamuzi aliwakatalia bao halali lakini akaongeza kwamba walipata nafasi kadhaa wakashindwa kuzimalizia.