*Manchester City wavuka mabao 100
Wakati Arsenal wakiamka kipindi cha pili na kuwapiga Fulham 2-0, Manchester City wameendelea kuwakimbilia kwa kufikia rekodi ya mabao 100.
Arsenal wakicheza nyumbani walibanwa na Fulham katika kipindi chote cha kwanza kiasi cha kwenda suluhu mapumziko.
Vijana wa Arsene Wenger, hata hivyo, walionesha nia yao ya kutwaa ubingwa waliporejea, ambapo ndani ya dakika tano walifunga mabao mawili kupitia kiungo Santiago Cazorla.
Mhispania huyo alifunga mabao yake mazuri katika dakika ya 57 na 62 na kuifanya timu yake kupata ushindi wa tano mfululizo katika mechi kubwa na kubaki nafasi ya kwanza walau kwa mzunguko huu tena.
Fulham walionesha kujiamini chini ya kocha wao mpya, Rene Meulensteen aliyechukua nafasi ya Martin Jol na nusura Steve Sidwell atikise nyavu za Gunners kama si kazi ya ziada ya kipa Wojciech Szczesny.
Katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na watazamani 60,000, hapakuwa na kadi yoyote iliyotolewa na mwamuzi Lee Probert, iwe ya njano au nyekundu.
Arsenal sasa wameruhusu mabao matatu tu katika mechi 10 walizocheza nyumbani wakati Fulham wapo pointi moja tu juu ya mstari wa timu zinazoshuka daraja, hali yao mbaya ikizidishwa na kufungwa 4-1 na Sunderland wiki iliyopita.
Kocha Wenger alisema shinikizo lipo kwao lakini wataendeleza umoja walioonesha tangu mwanzo kwa kuendeleza mchezo wanaoutaka na kujikusanyia pointi zaidi.
Man City kwa upande wao waliwapachika Cardiff mabao 4-2 baada ya kubanwa pia katika kipindi cha kwanza.
Mabao ya vijana hao wa Manuel Pellegrini yalifungwa na Eden Dzeko, Jesús Navas, Yaya Touré na Sergio Agüero wakati yale ya Cardiff yalifungwa na Noone na Campbell.
Jumamosi hii pia, Liverpool walikomboa mabao mawili waliyokuwa wamefungwa na Aston Villa na kutoka sare ya 2-2.
Mabao ya Aston Villa yalifungwa na Weineman na Christian Benteke wakati ya Liverpool yalifungwa na Daniel Sturridge aliyerejea kutoka kwenye majeraha katika dakika ya 45 na Steven Gerrard akasawazisha kwa penati baada ya Luis Suarez kuanguka kutokana na mkabiliano na kipa Brad Guzan.
Katika mechi nyingine, Newcastle waliwachapa West Ham 3-1 na kuzidi kuwatia matatani katika msimamo wa ligi na kumpa wakati mgumu kocha Sam Allardyce.
Norwich walipata ushindi muhimu dhidi ya wageni wa ligi kuu, Hull, walipowafunga 1-0 na kumpa raha kocha mweusi pekee katika ligi hii, Chris Hughton.
Crystal Palace walifanikiwa kuwafunga Stoke 1-0 wakati Sunderland wakicheza nyumbani walikwenda sare ya 2-2 na na Southampton.
Jumapili hii mtoto hatumwi dukani, kwani Manchester United walioanza ligi kwa wakati mgumu watataka kudhihirisha kwamba wao wamekuwa ni zaidi ya wengine watakapokutana na Chelsea katika uwanja wa Stamford Bridge.
Kadhalika Swansea watawaalika Totteham Hotspur nchini Swansea na Jumatatu mzunguko huu wa 22 utaendelea kwa mechi baina ya West Bromwich Albion na Everton.
Comments
Loading…