Tanzania inakwenda kuandika rekodi yake mpya katika upande wa kandanda. Kuna kila sababu za kujivunia uenyeji wa mashindano ya CHAN mwaka huu na kuwapa raha wapenzi wa soka. Bila shaka yoyote CAF wanaelewa namna watanzania walivyo wagonjwa wa mchezo w ampira wa miguu, kifupi hawaambiliki kama Wabrazil. Kama kuna nchi ambayo imejaa washabiki kindakindaki wa mchezo wa soka basi Brazil ni mfano wetu mzuri kwa nchi inapokuwa mwenyeji. TANZANIASPORTS inakuletea sababu muhimu kwa Watanzania kuzitukuza fainali za CHAN 2025.
CAF wanalitaka ‘vibe’ letu
Shirikisho la soka Afrika CAF kwa kushirikiana shirikisho la Soka Dunia FIFA waliandaa ufunguzi wa Afican Football League katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar Es Salaam. Lile shangwe la mashabiki kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho pamoja na Ligi Kuu ndiyo sababu hasa inayowafanya viongozi wetu kutamani mechi nyingi zichezwe hapa nchini. Ingawaje kanuni zinasema kila nchi inayochaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON lazima waandae mashindano ya CHAN kabla, ni dhahiri soka la Tanzania na mashabiki wake wanatamaniwa sehemu nyingi Afrika. CAF bila kupepesa macho wanalitamani sana ‘Vibe’ la mashabiki wa soka nchini. Lile shangwe unaliona kwenye Kariakoo Derby, Mzizima Derby au michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho pamoja na michezo ya Timu za Taifa, ni kielelezo kuwa mashabiki wetu wanajua maana na umuhimu wa kujaza uwanja. Kwahiyo CAF wana uhakika wa viwanja vyake nchini hapa kujazwa na mashabiki pomoni. Iwe New Amaan Complex visiwani Zanzibar au Benjamin Mkapa jijini Dar Es Salaam, CAF wanalipenda ‘Vibe’ hili na lazima mashabiki tukakidhi vigezo na kuwatamanisha wengineo huko Afrika na duniani. Twendeni kwenye CHAN 2025 tukazaje viwanja vyetu vyote viwili.
Uchizi wa soka tunao, tunatamba Afrika
Wakati tukiingia kwenye mashindnao ya CHAN ni muhimu wadau na mashabiki kuwaambia wenzetu barani Afrika kuwa tunao uwezo wa kujaza viwanja vyetu hata kama kutakuwa na mechi nyingi kubwa Barani Ulaya. Kwamba katika soka la nyumbani hatuna masihara nalo na viwanja vyetu vinakwenda kujazwa. Wabrazil wanapoandaa mashindano yao, hawana jambo dogo. Kwao kila mechi lazima ijaze uwanja. Haijalishi wanacheza Maracana, au kule Belo Holizonte, ama kokote kama Sao Paulo, Rio De Janeiro na miji mingine. Wabrazil wanaupenda mchezo wa soka, kama ambavyo watanzania wanavyoupenda. Wabrazil licha ya kuwa na wachezaji wengi barani Ulaya na Asia pamoja na Afrika bado wanatazama na kujazana kwenye viwanja kwa ajili ya mechi za nyumbani kwao. Ligi yao imejaa mashabiki, kila kiwanja ni sehemu ya burudani. Mpira ni mali ya wote, matajiri na masikini. Hali hiyo ndiyo inayotawala Tanzania. Katika mitandao mbalimbali picha za mashabiki wa Tanzania waliojanzana viwanjani ni kitu cha kawaida. Mijadala ya mitandaoni kwa nchi mbalimbali Afrika na hata vilabu vinavyokuja hapa vinaelewa kuwa watanzania wamechizika kwenye mpira wa miguu, kifupi huwaelezi kitu. Timu zao ndicho kitu cha kwanza, kisha ligi za ughaibuni ni kitu cha pili. Tanzania ni nchi inayohusudu soka lao, wachezaji wao na zaidi uenyeji huu unakwenda kuwapa burudani watu watakaotazama kwa njia ya televisheni kwamba usicheze na mashabiki wa Bongo.
Turufu yetu ya AFCON
Kwenye mashindano ya CHAN tunakoshirikiana na majirani zetu Kenya na Uganda, vinahitajika viwanja sita kamili. Kenya wanatakiwa kuwa kamili na viwanja viwili. Uganda nao wanatakiwa kuwa kamili na viwanja viwili. Tanzania hali kadhalika. Kuwa mwenyeji wa CHAN ni sehemu nzuri ya kuonesha utayari wan chi zetu na namna mashabiki wanavyonogesha michezo hiyo. Ni wazi kwenye mashindnao ya CHAN mwaka huu mashabiki wanakwenda kuzifurahisha nyoyo za wageni. Michuano hii tunapaswa kutumia kama nyenzo ya kutangaza soka letu, vipaji vyetu, fursa zetu na uhondo utokanao na mashabiki wetu. Hakuna kitu kizuri kwenye soka kama uwingi wa mashabiki wanaolipia tiketi na kujazana viwanjani. Hivyo basi CAF wanatamani ‘vibe’ la mashabiki wetu.
Bao la Mama
Bila shaka kwa mara nyingine serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan itaweka vitita vya bao la mama. Sifahamu itakuwa kiasi gani kwa kila bao watakalokuwa wanafunga vijana wa Taifa Stars ama itatumika njia ileile wanayolipa kwa klabu zetu zinashiriki mashindano ya CAF. Bao la mama lina mchango wa kuamsha ari na ushindani zaidi. Bila shaka wachezaji na benchi la ufundi wamejiandaa kwa ajili ya kushuhudia mabao ya mama yakifungwa kwa swaga na madoido mbalimbali. Je nani atatangulia kutufungulia bao la mama? Bila shaka wachezaji wetu hawatatuangusha.
Haya, twendeni tukavijaze viwanja vyetu kama wafanyavyo Wabrazil.
Comments
Loading…