WAPO watu wanaoshangazwa na kitendo cha Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) kuwapa Guinea ya Ikweta, moja ya nchi ndogo zaidi barani uenyeji wa michuano mikubwa ya AFCON kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha miaka minne.

Pamoja na ukweli kwamba walishatolewa kutokana na kuchezesha mchezaji asiye na sifa kwenye hatua za awali, kupewa kwao uenyeji baada ya Morocco kutaka tarehe iahirishwe kwa karibu wiki mbili hadi Februari mwakani, kuna sababu za kisiasa nyuma ya uamuzi huu.

Guinea ya Ikweta ni moja ya nchi zilizokwishatiwa alama nyekundu na mbaya kwa mwenendo wake katika rushwa duniani, na rais wake, Teodore Abiang Nguema Mbasogo ndiye mtawala wa muda mrefu zaidi miongoni mwa nchi za Afrika.

Mbasogo ametawala nchi hii yenye watu 740,000 lakini yenye utajiri mkubwa wa mafuta kwa miaka 32 na anaendelea kutawala, ambapo katika kuonesha jeuri yake, ameamua kuchukua uenyeji huo, kama alivyofanya wa viongozi wa Umoja wa Afrika (AU), ambapo alikuwa mwenyeji na aliwaandalia mkutano katika mazingira ya kifahari sana miaka ya karibuni.

Morocco walipotangaza nia yao ya mashindano kuahirishwa, Kiongozi wa Caf, Issa Hayatou alisema piga ua lazima michuano ifanyike katika tarehe zilizopangwa, vinginevyo Afrika ingeingia katika hali ngumu.

Caf ilihaha kuokoa mashindano hayo, na inaelezwa kwamba iliwasiliana na baadhi ya nchi ambazo ama zilikataa au zilishindwa kutokana na mazingira yenyewe kuwa ya ghafla, hata kama zilishaomba awali kuandaa AFCON 2015.

image

Nchi za Afrika Kusini walioandaa fainali hizo mwaka jana, Algeria na Sudan wanaaminika kuwakatalia Caf huku Ghana walioziandaa 2008 na Nigeria walivutiwa maombi ya Caf lakini hatimaye wakakataa.

Uwezekano mwingine ulikuwa kwa Angola waliokuwa wenyeji wa mashindano hayo 2010, matajiri wengine wa mafuta, lakini baada ya tafakari wakakataa licha ya kwamba wana miundombinu inayotakiwa. Muda ni mfupi lakini pia bajeti haikuwa imetengwa, hata kama fedha zipo.

Baada ya kupelekesjwa hivyo, Caf wakaona wazi kwamba kinachotakiwa si tu nchi kuwa na miundombinu, bali lazima utashi wa kisiasa uwepo, na haikuchukua muda, Hayatou akapanda ndege hadi Malabo, makao makuu ya Guinea ya Ikweta, akapata miadi na rais na dili likakubalika.

Mwaka 2012 Guinea ya Ikweta walikuwa wenyeji wenza na Gabon kwa ajili ya fainali hizo na sasa wanaziandaa wenyewe.

Haijajulikana Transparency International, chombo kinachomulika mlungula duniani kitatoa kauli gani juu ya uamuzi huo.

Inaelezwa pia kwamba nchi hii yenye ukubwa wa kilometa 28,000 za mraba, inaongoza kwa ukiukwaji wa haki za binadamu, ambapo inaelezwa watoto na wanawake wengi huenda huko kwa ajili ya kufanya kazi kitumwa na kuhujumiwa kimapenzi.

Kiasi kikubwa cha utajiri wa nchi hiyo kinamilikiwa na tabaka la watawala, rais mwenyewe akitajwa kujichotea kiasi cha kutisha. Iwapo mgawanyo wa fedha za mafuta ungekuwa sawa, ingekuwa moja ya nchi zenye watu tajiri zaidi duniani.

Mgawanyo sawa ungempatia kila mwananchi dola 30,000 za Marekani kwa mwaka, na kwa 2008 ingekuwa ya 20 kwa hali njema zaidi za watu wake duniani, lakini kutokana na rushwa, ufujaji na madhila mengine, ni ya 121 kati ya nchi 177 zilizoorodheshwa kwenye ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya maendeleo ya watu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Mancini bosi mpya Milan

Cristiano Ronaldo na rekodi mpya