*Haki yatendeka baada ya Waburkinabe kuminywa
*Nigeria wawashangaza Mali kwa kipondo kikubwa
Historia imewekwa Afrika Kusini, kwa Burkina Faso kuingia fainali ya michezo ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Burkina Faso waliovuka vigingi vingi, wameisukuma nje Ghana na sasa watacheza fainali dhidi ya Nigeria waliocharuka na kuwapa Mali kichapo cha mabao 4-1.
Waburkinabe walicheza kufa na kupona katika dakika 90 za kawaida na ilikuwa kama walikosa bahati hadi dakika 30 za ziada.
Wakicheza dhidi ya Ghana waliokuwa wamefufua matumaini ya kutwaa kombe, ikiwa ni ahadi wachezaji waliowapa wananchi wao, Burkina Faso waling’ara.
Hata hivyo, kulikuwa na ukatishaji mwingi wa tamaa kutoka kwa mwamuzi na wasaidizi wake, kwa jinsi walivyonyimwa fursa au wapinzani wao kupewa katika mechi iliyofanyika Nelspruit.
Burkina Faso walinyimwa penati za wazi katika muda wa kawaida na ule wa ziada, ambapo badala yake mchezaji aliyeangushwa kwenye eneo la hatari, Jonathan Pitroipa alipewa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje.
Pitroipa ni mmoja wa wachezaji mahiri zaidi wa mashindano haya, na iwapo hakuna hatua zitakazochukuliwa kubadili uamuzi huo, atakosa fainali ya Jumapili hii.
Nyota ikionekana kuing’aria Ghana kwa muda mwingi wa mchezo, walau katika kuzuiwa kuadhirika, walitangulia kupata bao kwa penati tata dakika ya 13 iliyofungwa na Mubarak Wakaso.
Hata hivyo, jitihada za Burkina Faso zilizaa matunda, kwani Aristide Bance alisawazisha katika dakika ya 60.
Dakika za mwisho za muda wa ziada zilishuhudia Waburkinabe wakijipanga vyema, kuingia hadi eneo la hatari la adui, lakini mlango ukawa mgumu.
Timu ziliingia kwenye mikwaju ya penati zikiwa na sare hiyo hiyo, ndipo hatimaye mwenye haki akapewa, kwa Burkina Faso kuwatoa Ghana kwa jumla ya penati 3-2.
Nigeria kwa upande wao, waliserereka kirahisi kupata ushindi dhidi ya Mali waliotarajiwa kuweka ushindani mkali.
Nahodha wa Mali, Seydou Keita alishawaahidi ushindi wananchi wake wanaoshuhudia mapigano kaskazini mwa nchi yao, lakini walishindwa kuweka ahadi katika vitendo.
Nigeria walipata mabao yao kupitia beki Elderson Echiejile aliyekwamisha kimiani majalo ya Victor Moses anayekipiga Chelsea.
Bao la pili lilifungwa na Brown Ideye aliyemhadaa golikipa wa Mali, Mamadou Samassa, huku bao la tatu likifungwa na nyota wao, Emmanuel Emenike kwa mpira kumparaza kiungo wa Mali, Momo Sissoko.
Mchezaji wa akiba, Ahmed Musa aliyechukua nafasi ya Victor Moses dakika ya 53, alifanikiwa kuwadungua Mali bao la tatu, kabla ya Cheick Diarra kupata bao la kufutia machozi dakika ya 75.
Nigeria wanaingia fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2000, wakijaribu kutwaa kombe walilolipata mara ya mwisho 1994. Wameshatawazwa wafalme wa soka ya Afrika mara tatu.
Comments
Loading…