in , ,

BURIANI DIOUF WA MARSEILLE:

BURIANI DIOUF WA MARSEILLE:

Jasiri aliyebadili soka Ufaransa

Ni ngumu sana kuandika juu ya umuhimu wa mtu mmoja wakati wa janga lisilo la kawaida, lakini nitajitahidi kufanya hivyo, kwa kuvuta kumbukumbu na hisia kadhalika.

Leo tunaye Pape Diouf, kiongozi jasiri asiye na chembe ya woga, aliyepambana kuisuka na kuifanyia mabadiliko makubwa na chanya soka ya Ufaransa, nchi jirani na hapa Uingereza.

Nasema tunaye kwa maana ya tunamkumbuka pamoja na mengi aliyoyafanya, lakini ukweli ni kwamba nguli huyu na shujaa wa soka ametangulia mbele ya haki, baada ya kuambukizwa virusi vya korona, akashambuliwa na uhai kutoweka kwa homa kali ya mapafu, akiwa na umri wa miaka 68.

Diouf ameacha alama kubwa kwenye soka na wadau daima wataienzi; alikuwa rais wa kwanza mweusi wa klabu ya daraja la juu kabisa hapa Ulaya. Wakati ulipofika, alijitokeza, hakuogopa, akaongoza kwa ujasiri mkubwa akipangua vikwazo vingi mbele yake na kufanikiwa.

Maisha ya mweusi huyu tunayemjivunia yamestahili kabisa kutazamwa, kutambuliwa na kuweka kile tunachoweza kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye. Akiwa amezaliwa nchini Chad na wazazi ambao ni wa Senegal – Afrika Magharibi, Diouf alihamia Marseille akiwa na umri wa miaka 18.

Aliingia Marseille – Ufaransa kwa nia ya kuwa na kufanya kazi ya uaskari kama wazazi wake walivyomwagiza, lakini mwenyewe akawa mahiri kubadili njia yake, akateka fursa zilizojitokeza mbele yake na hata ambazo alitakiwa kuzitafuta nchini Ufaransa kama wasemavyo mtaka cha uvunguni lazima ainame.

Kwa aibu kubwa mbele ya wazazi wake, Diouf alianza kufanya kazi ofisi ya posta, akiachana na masomo kwa ajili ya nafasi iliyojitokeza mara moja akaona asiiache. Safari yake ilisaidia kumjenga kuwa imara na hata mwenendo butu pasipo kuogopa.

Alisonga mbele bila wasiwasi huku akijiamini sana, akaja akawa wakala wa soka – hii ikampaisha na kumfanya si tu mtu mwenye ushawishi mkubwa bali mtu mmoja muhimu sana kwenye sekta.

Hakuishia hapo; kwa miaka kadhaa amefanya kazi kama mwanahabari upande wa kusini mwa Ufaransa, akijielekez zaidi kwenye habari za mji wa bandari wa Marsaeille kwa ajili ya ‘La Marseillaise’, kwanza akiwa kama mwandishi huru, kisha akaja kuajiriwa na kuwa ripota kiongozi wa gazeti hilo, kabla ya kuhama na kujiunga na gazeti kubwa zaidi la kitaifa la michezo lililokwenda kwa jina la ‘Le Sport’.

Ilikuja kutokea kwamba kampuni ya gazeti hilo ilifilisika, ikabidi Diouf ‘apige akili’, akatumia mtandao aliokuwa nao na wachezaji wa klabu ya soka ya Marseille ndiposa akaanza kuwa wakala. Alijiongeza kila kukicha akasonga na kupanda kuja kuwa mtu mzito mwenye mvuto, ushawishi na hakika mwanamapinduzi kwenye ulimwengu wa soka.

Huyu ni mtu aliyetokea kuwa mithili ya mvunja mwamba usiotarajiwa kuwezekana, mtu wa ukweli enzi ambazo mawakala wa soka hawakuwa na nguvu kama sasa na haikuwa kawaida kwa watu weusi, tena wazaliwa wa Afrika kabisa kuwa kwenye sekta hiyo, achilia mbali kuwa na ushawishi.

Basile Boli na Joseph-Antoine Bell – wote wakiwa walichezea Marseille wakati huo ndio wateja wake wa kwanza. Klabu ilipanda na kuwa katika mafanikio makubwa mwaka 1993 wakitwaa pia kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL). Boli ndiye alikuwa shujaa kwenye fainali hiyo ya UCL kwa kufunga bao dhidi ya Milan, akiwa anatoka Ivory Coast katika umri mdogo na kuwika Ufaransa.

Diouf alionekana kama baba kwa mlinzi huyu. “Siwezi hata kuzungumza. Huyu si rafiki tu – alikuwa kama mzazi au kaka mkubwa kwangu. Watoto wangu wote, mama na baba yangu walimjua na kumpenda sana,” ndiyo maneno ya Boli baada ya kusikia juu ya kifo cha Diouf.

Huku kukiwa na mafanikio makubwa kwa wateja wake Marseille – walipokonywa kombe ambalo ilidaiwa kwamba walihonga. Wasingepokonywa, ubingwa wa msimu wa tatu mfululizo. Potelea mbali, nyota ya Diouf ilianza kung’ara hasa.

Drogba
Drogba alilelewa na DIOUF WA MARSEILLE

Grégory Coupet, Marcel Desailly na Bernard Lama mara wakamteua kuwa wakala wao, akisaidiwa kwa kiasi kikubwa na intelijensia, haiba ya mvuto na ushawishi vilimsaidia kukua haraka miongoni mwa watu wazito waliokuwa katika mamlaka au uwezo wa kuwaingiza wengine humo.

Alilielewa gemu vyema na sasa alianza kuwa kimataifa zaidi, akiwa na wachezaji kama Didier Drogba, Laurent Robert na Desailly wakifanya vyema, mikono ya Diouf ilisogea hadi hapa England ambako yeye na Arsene Wenger – kocha wa zamani wa Arsenal, walifanya makubwa kuleta wachezaji waliokuwa na vipaji vikubwa vya soka kutoka Ufaransa.

Mmiliki wa Marseille, Robert Louis-Dreyfus alimwajiri Diouf kuwa mkurugenzi wa soka wa klabu hiyo 2004 kutokana na mtandao mkubwa aliokuwa nao. Jose Anigo alipojiuzulu ukocha baadaye mwaka huo, Diouf alipewa urais wa klabu, akichukua nafasi ya Christophe Bouchet aliyejikuta katika hali mbaya kiuongozi.

Wachezaji wengine aliotamba nao ni pamoja na Franck Ribéry, Mamadou Niang, Samir Nasri aliyekuwa anaibukia. Wengine ni Steve Mandanda, Hilton, Karim Ziani na Bakari Koné. Baada ya kukaa wadhifani kwa mafanikio makubwa, Diouf aliondoka na kwenda kufanya kazi kwenye Chuo cha Uandishi wa Habari lakini aliingia pia kwenye siasa za jiji hilo.

Niseme tena, kifo chake ni mojawapo ya vingi vinavyotokea duniani wakati huu wa janga la virusi vya corona, lakini kwa mtu aliyepita kote huko kutafuta maisha mazuri kwake na familia na marafiki, amestahili kutazamwa na kuelezwa hivi. Alikuwa mtu wa daraja la aina yake, mwenye heshima kijamii na kisoka na ataendelea kuheshimiwa, tukiyaishi yale aliyoamini, kupigania na kusimamia, akiwa hana mpaka wa jambo – ila mbingu. Pumzika kwa amani Pape Diouf.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Muda huu Ngassa angekuwa China anakula mafao

Tanzania Sports

Kabla ya kumsajili Makambo, Mleteni Yusuph Mhilu