Je, unaweza kumpenda kocha peke yake bila timu anayofundisha? Hilo ndilo limewahi kunikuta mimi kila nilipotazama timu inayofundishwa na Brendan Rodgers. Kaa kitako msomaji nikusimulie sababu za kupenda ufundishaji wa Brendan Rodgers.
Kwanza ni kocha ambaye kwa sasa anahusishwa na mpango wa kuajiriwa kufundisha Manchester United. Kuajiriwa kwenye timu kubwa na yenye historia kabambe kama Manchester United ni sifa kubwa na inampa nafasi ya kuonesha umahiri zaidi.
Kama ningekuwa mshauri wa Manchester United ningewaambia wamchukue kocha huyu na ninazo sababu nyingi mno na anamzidi Ole Gunnar Solskjaer kwa mbali sana.
Miaka kadhaa iliyopita Brendan Rodgers alikuwa anafundisha Swansea City. Kabla ya ukocha wake hapo alikuwa mwanafunzi wa kocha gwiji Jose Mourinho kipindi alichokuwa akiinoa Chelsea.
Kwahiyo Brendan Rodgers amejifunza ukocha nje ya darasa kupitia Jose Mourinho mbali ya vyeti vyake halisi. Mourinho alipoondoka Chelsea alikuja kuzinoa Inter Milan, Real Madrid, Manchester United na Tottenham Hotspurs.
Kwangu mimi Rodgers ana kitu cha aina yake, ni mwalimu ambaye anafundisha soka ninalopenda. Timu icheze kwa pasi fupi fupi kwa kasi, kutawala mchezo na kupata ushindi. Yaani timu iwe inacheza soka la kutafuta pointi au ushindi huku ikiwa inawapa burudani.
Si kama anavyofundisha Pep Guardiola pasi zinakuwa nyingi wakati mwingine unaona wazi mipango yake inafeli na haiwezi kumleta pointi. Kwa Brendan Rodgers nilipenda namna alivyoifanya Swasea City itandaze soka maridadi na kwa hakika ilikuwa timu inayovutia kuitazama.
Kuna wakati makocha wanatuvutia sisi mashabiki kutazama timu zao namna zinavyocheza,kusaka ushindi na burudani anuai. Wakati akiwa kocha wa Liverpool kulikuwa na presha kubwa ya kutwaa ubingwa.
Na makosa ya nahodha wao Steven Gerard kwenye mchezo dhidi ya Cheslea ya Mourinho yakamkosesha taji Brendan Rodgers. Liverpool ilikuwa inacheza soka maridadi,pasi nyingi,kutawala mchezo na ushindi wake ulikuwa unavutia.
Timu ya Brendan Rodgers inacheza kwa ari mno, uchu wao wa kupata ushindi unakuwa umepangiliwa na namna timu inavyojijenga na kuwa tishio ndipo ninapoona umahiri wa kocha huyo. Anafundisha mpira ambao unawapa wachezaji nafasi ya kupumua.
Kwa ufundishaji wake hana kasi ya mchezo muda wote lakini timu zake huwa zinavutia kuzitazama. Alipokuwa kocha wa Celtic ya Uskochi nako alikuwa na mtindo uleule kuhakisha timu inacheza kandanda safi na kupata ushindi ukiwa umewakosaha mashabiki.
Wakati fulani niliwahi kuandika kwenye moja ya kolamu zangu za Madridista kuwa natamani siku moja Brendan Rodgers angekuja kuwa kocha wa Real Madrid.
Niliamini ni kocha ambaye ana kila sifa za kufundisha timu kubwa ikiwa ataachiwa utulivu na kupewa muda wa kutosha kwenye hizi timu kubwa. Presha ya timu kubwa wakati mwingine zinawaumiza makocha hivyo baadhi hukaa muda mfupi kabla ya kufukuzwa.
Mtazame Julen Lopetegui wa Sevilla alivyotulia na timu na huwezi kudhani ndiye kocha aliyefukuzwa Real Madrid. Mtazame Emery Unai alivyotulia Villareal huwezi kudhani ndiye aliyeondoka PSG an Arsenal. Kwahiyo kwa Brendan Rodgers kupewa kibarua cha Manchester United, binafsi natamani mno kumwona akiwa timu kubwa zaidi ya Liverpool iliyoko kwenye wasifu wake (CV).
Kwa sasa anao uzoefu wa kufundisha timu za aina mbili; kwanza timu zenye bajeti kubwa na wachezaji wakubwa na timu ndogo zenye bajeti ndogo lakini zikafanya mambo mazuri. Kuifundisha Swasea City si sawa na
Liverpool wala Leicester City si sawa na Celtic au kama atapewa Manchester United. Kwa bajeti Liverpool ni zaidi ta Celtic,Leicester na Swansea.
Tangu alipoichukua Leicester City ameifanya timu hiyo kuwa ngumu,yenye utulivu na kucheza kwa mipango ambayo inaonekana wazi. Kuna wakati unaweza kusema anakosa wachezaji wenye vipaji vikubwa au bajeti kubwa ya kusajili wachezaji.
Kwa wachezaji alionao ndio ametwaa taji la FA na Ngao ya Jamii. Ni kocha ambaye amemsumbua Pep Guardiola na mastaa wake ambao walishindwa kufurukuta mbele ya Leicester City kwenye fainali ya FA.
Rodgers ana miaka 48 tu na dhahiri muda anao na uchu wa kushinda mataji bado anao. Kwahiyo kama Manchester United hawana kisingizio kingine zaidi ya kumpa timu mtu huyu na kumwondoa pale King Power stadium.
Furaha ya Brendan haitakuwa kuifundisha Manchester United tu bali kuona kocha huyo hatimaye maono yangu kuwa anastahili kupewa klabu kubwa na ambayo alitakiwa kuipata mapema kabla ya Ole Gunnar Solskjaer.
Matamanio yangu ni kuona anazinoa timu kubwa kutokana na umahiri wake kwenye mchezo huo. Ni mapenzi kwake lakini timu pekee ambayo natamani angekuwa nayo ni Real Madrid tu, kwanza anajua kvaa suti, ametulia, hana mengi nje ya uwanja,hana kelele kwenye vyombo vya habari, sio mtengeneza habari kama walivyo makocha wengine maarufu. Kifupi ametulia mno, ukiongeza na uwezo wake wa ufundishaji unavutia mno ingawa sio kila wakati unaweza kuipatia taji timu yake.
Comments
Loading…