in , , ,

Brazil waanza kwa ushindi

*Ni baada ya Croatia kuwapelekesha

Brazil wamefanikiwa kuwatoa kimasomaso washabiki wake kwa kushinda mechi ya ufunguzi wa michuano ya Kombe la Dunia.
Samba Boys au Selecao walitoka nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Croatia na kushinda 3-1 huku wakipewa penati tata wakati matokeo yakiwa 1-1 na kuwakasirisha Croatia.
Hata hivyo, mabao yote manne yalifungwa na wachezaji wa Brazil, kwani Marcelo alianza kwa kujifunga mapema dakika ya 11 kabla ya Neymar kusawazisha dakika ya 29, penati dakika ya 71 na Oscar kumaliza mambo dakika ya 90.

 

Katika mechi iliyochezwa jijini Sao Paulo baada ya sherehe kabambe za ufunguzi, Neymar aling’ara kama ilivyokuwa imetabiriwa.
Oscar alikuwa hapewi nafasi ya kufanya vyema sana kutokana na kiwango chake Chelsea lakini bao lake lilikuwa zuri, tena kutokana na jitihada binafsi.

 

Mwamuzi wa Japan, Yuichi Nishimura alitoa penati tata kwa madai kwamba Dejan Lovren alimchezea rafu Fred ndani ya eneo la hatari licha ya kuonekana kwamba mgusano ulikuwa kwa mbali kidogo.
Huu ni ushindi wa 10 mfululizo kwa Kocha Luiz Felipe Scolari ‘Big Phil’ ambaye timu yake inapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele na hata kutwaa ubingwa, ambapo ametabiri watacheza fainali na Argentina.

 

Hata hivyo, Brazil hawakucheza soka ya kupamba, mbwembwe na kuvutia kama ile waliyoonesha walipowafunga Hispania kwenye fainali ya Kombe la Mabara mwaka jana.
Brazil walionesha uzalendo wa hali ya juu wakati wa kuimba wimbo wao wa taifa huku Croatia wakijitoa kwa hali na mali wakiungwa mkono na maelfu kidogo ya washabiki waliosafiri kutoka kwao.

 

Wakicheza bila Mario Mandzukic ambaye Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alikuwa uwanjani kumtazama kwa kuwa ananuia kumsajili, Croatia walimtumia vyema Ivica Olic aliyefanya kazi bila kuchoka na kuwapa tabu mabeki wa Brazil.

Nusura afunge bao katika dakika ya saba kwa kichwa alipotumbukiziwa majalo na Ivan Perisic kutoka upande wa kulia na dakika nne baadaye aliwanyamazisha Wabrazil kwa mwenendo wake wa kutisha.
Ni yeye aliyemtoka Dani Alves akaachia majalo iliyomkuta Nikica Jelavic aliyepiga mpira ambao ulimgonga Marcelo na akiwa hana la kufanya ukatumbukia kwenye nyavu za timu yake huku kipa Julio Cesar akishindwa kuzuia.

 

Brazil walipelekeshwa wakaonekana kushindwa kwenda na kasi ya Croatia na nusura siku iwatumbukie nyongo pale Neymar alipompiga Luka Modric usoni akaambulia kadi ya njano; angeweza kupata nyekundu.
Ijumaa hii Cameroon watacheza na Mexico, Hispania na Uholanzi na Chile watakipiga dhidi ya Australia katika siku ya pili ya michuano hiyo mikubwa zaidi duniani.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Uzinduzi wafana Brazil

TETESI ZA USAJILI