in

Bosi wa Simba na taswira ya wanawake katika michezo

Barbara Gonzalez

Barbara Gonzalez ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa mkubwa ngazi ya klabu nchini Tanzania. Tangu kuteuliwa kwake kushika wadhifa wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa mabingwa hao wa soka, Barbara hakuwa amezungumza na vyombo vya habari. 

Gumzo kubwa liliibuka juu ya uteuzi wake. Lakini ukweli uliopo sasa Barbara ndiye bosi wa Simba na msimamizi wa shughuli za kila siku za klabu hiyo. Ndiye mtu anayetakiwa kuifikisha Simba katika viwango vya kimataifa kuanzia mafanikio ya mchezo pamoja na biashara kuuza na kununua wachezaji wakubwa na wenye vipaji. Bila shaka matanuzi sokoni na bajeti kubwa kuzikaribia TP Mazembe ya DR Kongo au Al Ahly ya nchini Misri. 

Kwa mujibu wa mahojiano aliyofanya na Shirika la Utangazaji la Uingereza Idhaa ya Kiswahili (BBC Swahili) ya hivi karibuni Barbara Gonzalez alizungumzia masuala muhimu ya uendeshaji wa taasisi za kijamii na namna alivyopata uzoefu wa kuwa mtendaji mkuu huko kabla ya kuafiki kushika madaraka ya kuongoza Simba. 

Aidha, wiki hii amekuwa gumzo zaidi kwenye vyombo vya habari baada ya kuanza kuzungumzia mikakati yake ya kuipaisha Simba kimataifa zaidi. Barbara amebainisha kuwa anataka Simba iwe na wanachama hai wanaolipia uanachama na kufanikisha kuingia mapato yatakayoisaidia timu hiyo kupaa zaidi

MWELEKEO WA BOSI WA SIMBA

Barbara Gonzalez amefichua kwa kusema, “Kama klabu itakuwa inaingiza fedha za kutosha, kwanini isiweze kumsajili mchezaji wa gharama kubwa ambao wataweza matokeo chanya ndani ya timu? Zamalek, TP Mazembe na klabu nyingine zinazotamba Afrika zimefika huko kwa vile zina uchumi mkubwa, kitu ambacho Simba ikikazana inaweza kufika huko na kutikisa Afrika,”.

Mwelekeo wa bosi huyo unatueleza kuwa Simba kama ilivyo kwa Yanga ni timu ambazo zinatakiwa kuwa na mikakati ya kidumu na kurithisha kizazi hadi kizazi juu ya maendeleo ya timu zao. Kukalia historia pekee ya ukombozi wa uhuru hakutoshi, ni lazima timu zifike mbali kimafainikio ikizingatiwa zimekuwa na miaka takribani zaidi ya 60 sasa. 

NAFASI YA WANAWAKE

Jambo moja muhimu Barbara Gonzalez anawakilisha taswira halisi ya wanawake wenye uwezo na nguvu katika mamlaka ya kuongoza taasisi mbalimbali. Mathalani, Tanzania kwa sasa ipo kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu wa 2020, hususani nafasi ya urais wapo wanawake wachache wamejitokeza; Queen Cathbert Sendinga na Cecilia Augustino Mwanga.

Tuchukue mfano wa taasisi za kisiasa zinazoongoza nchini Tanzania, tangu enzi  za uongozi wa Mwalimu Nyerere wanawake wengi walikuwa bado katika suala la kujiamini kushika uongozi wa ngazi zozote au kwenye vyombo vya uamuzi ndani ya nchi. Hii namaanisha hata katika ngazi za familia na katika kaya nyingi kama sio zote viongozi kwa asilimia kubwa walikuwa ni wanaume. Mambo yamebadilika kiasi kwamba wanawake wanaonekana kushika nyadhifa nyeti kwa sasa. 

WANAWAKE NA MAENDELEO YA MICHEZO

Uamuzi wa Simba kumkabidhi Barbara jukumu la kuongoza timu hiyo akiwa Ofisa Mtendaji mkuu ni ushahidi wa wazi kuwa mchakato wa maendeleo ya michezo nchini hayaweza kuwewaka kando wanawake. Historia inaonesha kuwa sekta ya michezo imewahi kupata wanawake wawili pekee walioongoza taasisi kubwa nchini. 

Mosi; Lina Madina Mhando, ambaye amewahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA). Chama hicho ndicho chenye mamlaka ya kusimamia maendeleo ya mchezo wa soka kwa upande wa wanawake kikiwa mwanachama wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Pili;  Joan Minja, amewahi kuwa rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT). Hilo ni shirikisho lenye dhamana katika mchezo wa ngumi nchini, ambapo mabondia,waamuzi na wadau wake wanakuwa chini ya usimamiziwa BFT. 

Maeneo hayo mawili yameonesha kuwa wanawake ni sehemu ya maendeleo ya michezo nchini, kwahiyo hawawezi kuachwa nyuma. Kwamba ili mchakato wa maendeleo ukamilike ni lazima pande zote ziwe sehemu ya kusaka mafanikio.

Simba imejaribu kuongoza njia kuhakikisha wanawake wanakuwa sehemu ya maendeleo ya mchezo wa soka. Ukizingatia nafasi ndogo kama zile za wasemaji wa vilabu vya soka wengi ni wanaume. Ingawaje hoja hapa ni uwezo na ufanisi wa kazi, lakini katika uwiano na kuleta mvuto katika mchakato wa maendeleo suala la jinsia pia linahusika.

Kwa maana hiyo Barbara anakuwa taswira ya wanawake namna wanavyochukuliwa kwenye madaraka. Kwamba gumzo liliposhamiri lilionesha kana kwamba nafasi ya Afisa Mtendaji mkuu ilikuwa mahususi kwa aajili ya wanaume pekee. 

Wanawake wanaombwa kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye michezo, kwa sababu wanayo mifano ya wenzao waliofanikiwa kikazi kwenye taasisi mbalimbali. Taswira nzruri ya uongozi kupitia wanawake itajengwa na wanawake wenyewe kwa kuchukua hatua.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Zinedine Zidane

Zidane apange wakongwe au chipukizi?

Tuisila Kisinda

Tuisila Kisinda anamkosa MAKAMBO