BONDIA wa timu ya taifa ya ngumi za ridhaa inayojiandaa na michuano ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Oktoba nchini India, Hamdan Issa jana alianguka mazoezini na kupoteza fahamu kutokana na njaa. Mabondia hao ambao wanaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa jijini Dar es Salam wamekuwa wakilalamikia serikali mara kwa mara kuwa haiwajali katika suala la vifaa na kuwapa kambi nzuri. Mwananchi ilizungumza na mabondia hao ambao walionyesha kusikitishwa na hali ya kambi yao ya sasa na kuiomba serikali iweze iwasaidie kuwapa kambi nzuri ya kufanyia mazoezi na kupewa chakula ili waweze kutimiza malengo yao. Nahodha wa timu hiyo, Joseph Martin aliiambia Mwananchi kuwa endapo wangekuwa pamoja kambini lazima wangekuwa wanafahamiana na matatizo ya kuanguka kwa sababu ya njaa yasingetokea. “Huyu mwenzetu (Issa) ameanguka na kupoteza fahamu kwa muda, lakini baada ya kupepewa alirejewa na fahamu na hiyo ilisababishwa na njaa, hebu fikiria kwa tatizo kama hili hata daktari hatuna. ‘’Huwezi jua ndugu yangu tunaishi vipi huko majumbani, lakini endapo tungekuwa kambini ya moja kwa moja tusingekuwa na wakati mugumu kama ilivyo sasa. “Hata kocha analalamikia mazoezi haya na amepanga kuonana na rais wa shirikisho ( BFT)ili kumweleza matatizo ya ukata yanayoikumba kambi yetu kwani hiko katika hali ngumu mno. “Viongozi wetu wanahangaika kila kukicha kutafuta wafadhili, lakini bado hawajafanikiwa tunawaomba wadau wajitokeze na kutusaidia,” alisema Martin. Timu hiyo imekuwa ikikabiliwa na ukata tangu kuanza kwa kambi yao ya wazi kiasi cha kukosa mahitaji muhimu wakati wa mazoezi yao. Ukata huo umesababisha kukosa daktari , dawa, maji na vifaa vya mazoezi kama punching bags, vikinga kichwa, vikinga ulimi pamoja na gloves. Huku matatizo hayo yakiwa ni kilio kikubwa kwa mabondia wa timu ya taifa, lakini bado hawajakata tamaa ikiwa ni pamoja na kuendelea na mazoezi magumu kwa ajili ya mashindano mbalimbali ya kimataifa. |
Comments
Loading…