Usain Bolt amedhihirisha kwamba bado ndiye mtu mwenye kasi zaidi duniani, baada ya kuibuka mshindi kwenye mashindano ya ubingwa wa dunia kwa mita 100 na mita 200 jijini Beijing.
Mwanariadha huyo wa Jamaica alionesha makali yake kwa kuanza kwa kasi kiasi cha kuacha pengo la kutosha baina yake na mpinzani wake mkubwa kutoka Marekani, Justin Gatlin, aliyeishia kufukuzuia medali ya fedha.
Vuta nikuvute hiyo ilifanyika katika uwanja wa Bird’s Net (Kiota cha Ndege) huku kukiwa na joto na hewa nzito na hadi wanamaliza mita 100 za kwanza, tayari kulikuwa na dalili kwamba Bolt hangeachia nafasi yake hiyo.
Bolt alimalizia mstari wa mwisho kwa kujidai, akiweka vidole gumba vya mikono kifuani mwake kuonesha ushindi, ambapo alifanikiwa kumaliza mbio hizo kwa sekunde 19.55 tu, akikimbia kwa kasi kuliko mtu mwingine yeyote duniani mwaka huu.
Alikuwa katika kiwango kizuri, ambapo alimwacha mshindani wake Gatlin nyuma, akamaliza mbio hizo kwa sekunde 19.74. Bolt alieleza furaha yake kwa kuwa bingwa wa dunia mara ya 10, hasa katika kipindi hiki ambapo watu walikuwa wakitabiri kwamba angefanya vibaya.
“Watu walidai kwamba ningeshindwa, lakini nilijiamini sana. Madhali kocha wangu hana wasiwasi basi mimi huwa mara dufu yake. Kuna watu, kama Waingereza, wananionesha upendo mkubwa, nami nitaendelea kukimbia kwa kasi kubwa,” anasema Bolt.
Raia wa Afrika Kusini, Anaso Jobodwana aliweka rekodi mpya kwa taifa lake kwa kumaliza mita 200 ndani ya sekunde 19.87, wakati Alonso Edwards wa Panama alishika nafasi ya nne.
Mwingereza, Zharnel Hughes, 20, ambaye hufanya mazoezi na Bolt nchini Jamaica, alijivunjia rekodi yake, kwa kumaliza mbio ndani ya sekunde 20.02 na kushika nafasi ya tano.
Hughes alizaliwa kwenye visiwa vya Anguilla vinavyomilikiwa na Uingereza, vikiwa Caribbean Mashariki na alipata uraia wa Uingereza Juni mwaka huu tu. Alishinda kwenye michuano ya kitaifa ya mchujo kwa staili ya aina yake, akatabiriwa kwamba angefanya vyema kimataifa pia.
Pamoja na hao wote kufurahia ilikuwa tisa, kwani 10 ilikuwa furaha kwa Bolt mwenyewe anayetia kibindoni medali ya 10, ambapo pia alishika nafasi ya kwanza kwenye mbio za mita 100.
Gatlin, 33, kwa upande wake, amerejea uwanjani baada ya kuwa amezuiwa kushiriki mara mbili kwa maelezo ya kutumia dawa za kuongeza nguvu. Alipata kutwaa medali ya dhahabu kwa mbio za mita 100 katika michezo ya Olimpiki ambapo alikimbia kwa sekunde 9.74.
Katika uwanja ule ule, Bolt amevunja rekodi iliyowekwa na Michael Johnson miaka saba iliyopita.
Comments
Loading…