Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa kusimamishwa kazi kwa siku 90.
Blatter anadai kwamba hajafanya kosa lolote hivyo haoni sababu ya kufungiwa na Kamati ya Maadili ya Fifa.
Blatter anachunguzwa na mamlaka ya Serikali ya Uswisi na Kamati ya Fifa juu ya kuhusika kwake kwenye mipango ya rushwa shirikani kwa miaka kadhaa.
Hatua ya kumsimamisha kazi ilichukuliwa Alhamisi hii, sambamba na Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke na Makamu wa Rais, Michel Platini ambaye pia ni mkuu wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa).
Rafiki na mshauri wa Blatter, Klaus Stohlker amesema kwamba tayari rufaa hiyo imewasilishwa kwenye Kamati ya Rufaa ya Fifa, akidai kwamba ana uhakika hatapatikana na hatia.
Blatter alishauriwa mapema kutogombea tena kwenye uchaguzi wa Mei na baada ya hapo kuachia ngazi mara moja, lakini alikataa, akidai alikuwa na kazi ya kuandaa mageuzi makubwa ndani ya shirikisho hilo.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha England, David Bernstein amekaririw aakisema kwamba Blatter alijidanganya na kujiharibia mwenyewe kwa kkaa kwa muda mrefu hivyo mamlakani.
Makamu wa Rais wa Fifa, David Gill, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha England, amemwandikia Kaimu Katibu Mkuu wa Fifa, Markus Kattner kuitisha mkutano wa dharura wa kamati ya utendaji.
Kwa muda huu ambapo Blatter ametupwa nje ya ofisi, Mkuu wa Shirikisho la Soka la Afrika (Caf), Issa Hayatou aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi, ndiye anaongoza Fifa.
Kamati ya Maadili ya Fifa ilichukua hatua ya kumsimamisha Blatter kwa siku 90, kuisha uchunguzi dhidi yake.
Blatter, 79, anatuhumiwa kuhusika kusaini na kutekeleza mikataba batili, ikiwa ni pamoja na kutoa hongo.
Pamoja na mambo mengine, anatuhumiwa kutoa hongo kwa rais wa sasa wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini ili ajitoe kwenye kinyang’anyiro cha urais wa shirikisho hilo, na Platini kujitoa.
Imekuwa ikidhaniwa kwamba Platini ndiye angechukua kiti cha Blatter kwenye uchaguzi uliotarajiwa kufanyika Februari mwakani, lakini kwa hali ilivyo, ni vigumu kufahamu kitakachojiri.
Huu ni mfululizo wa hatua zinazochukuliwa tangu polisi wa Uswisi kuwadaka maofisa saba wa Fifa jijini Zurich, kabla ya mkutano mkuu wa shirikisho hilo.
Wakati Uswisi wakifanya upelelezi kuhusu mlungula ndani ya Fifa, Marekani walitangulia kuchukua hatua na baadhi ya watuhumiwa tayari wametakiwa kupelekwa nchini humo kukabiliana na mashitaka yao.