Kampuni ya bia nchini TBL iliyokuwa inadhamini mashindano ya ligi ya mpira wa kikapu ya Kili RBA kupitia bia yake ya Kilimanjaro, imetangaza kujitoa rasmi kudhamini mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa bia ya Kilimanjaro inayodhamini mashindano hayo George Kavishe alisema kujitoa huko kudhamini mashindano hayo kumetokana bia ya Kilimanjaro kutumika katika udhamini wa zaidi ya michezo mitatu.
Alisema kwa sasa kampuni hiyo haiwezi kudhamini mashindano yoyote ya mpira wa kikapu kutokana na majukumu mengi yanayoikabili kampuni hiyo ambayo pia inadhamini timu za Simba na Yanga.
“Kujitoa kwetu kudhamini mashindano ya mpira wa kikapu sio ya ugomvi ila tumeangalia majukumu mengine yanayotukabili, na Kilimanjaro kama bia haiwezi kudhamini zaidi ya michezo mitatu,” alisema Kavishe.
Kampuni ya hiyo ya bia kupitia kwa bia yake ya Kilimanjaro imekua mdhamini mkubwa wa mpira wa kikapu hasa katika mashindano ya ligi ya Kili RBA kwa zaidi ya miaka minne ambapo walikuwa wakitoa fedha za zawadi pamoja pamoja na gharama za kuendesha mashindano hayo ikiwa ni pamoja na posho kwa timu shiriki.
Awali ilisemekana kuwa kampuni hiyo imejitoa kufuatia kutoridhishwa na matumizi ya chama cha mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BD) kwa fedha wanazozitoa kwa ajili ya udhamini huo.
Katika mashindano ya msimu uliopita TBL ilitoa kiasi cha Sh. milioni 60 ambazo zinadaiwa kutumiwa vibaya, na BD na kushindwa kuonyesha mchanganuo wa matumizi yake.
Comments
Loading…