Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera amewataka wanariadha wanaoshiriki mbio za kimataifa kutokubali kuingizwa kwenye matatizo ya kuhusishwa na uuzaji wa madawa ya kulevya kwani watakuwa wamejipotezea malengo yao ya baadaye.
Bendera alitoa kauli hiyo wakati wa ufunguzi wa mashindano ya 47 ya taifa ya mchezo huo yaliyofanyika kwa siku mbili kwenye uwanja wa Namfua mjini hapa, ambapo aliwataka wachezaji kuwa waangalifu na viongozi wao ili wasijitumbukize katika matatizo hayo.
Hivi karibuni mabondia wawili na kocha mmoja wa timu ya taifa ya Tanzania, EmmilianPatrick, Petro Mtagwa na Nassoro Michael walikamatwa nchini Mauritius walipokwenda kwa ajili ya kushiriki mashindano wakidaiwa wameingiza madawa ya kulevya yenye thamani ya sh. bilioni 1.7, ambapo sasa rais wa Chama cha mchezo huo nchini, BFT, Shabaan Mintanga ameshapandishwa kizimbani kwenye mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akidaiwa kuhusika na sakata hilo.
Hata hivyo, alisema serikali sasa imedhamiria kuendeleza michezo ukiwemo wa riadhaambao unaliletea sifa taifa mara kwa mara kwa kujenga viwanja vya kisasa, pia imeshatoa agizo maeneo yote ya shule za msingi na sekondari zote nchini kutengewa viwanja vya michezo mbalimbali ili kukuza vipaji vya wachezaji wanaochipukia.
Bendera aliumwagia sifa mkoa wa Singida kwa kuwa ndio ulikuwa wa kwanza kufanyika mashindano ya shule za msingi mwaka 1974, kuwa ndio wenye vipaji vingi vya wanariadha ambapo ametoa mfano wa Juma Ikangaa, Samson Ramadhani na Christopher Isegwe waliofanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali duniani.
Kwa upande mwingine Katibu Mkuu wa Chama cha riadha nchini, RT, Suleiman Nyambuialisema lengo la chama chake kuleta mashindano mkoani hapa ni pamoja na kuwaenzi wanariadha waliong’ara zamani, na pia kuibua vipaji vingine.
- SOURCE: Nipashe
Comments
Loading…