in , , ,

Bayern Munich mabingwa Ulaya

Kwa mara ya tano katika historia, Bayern Munich wameutwaa ubingwa wa Ulaya, na kuwa zawadi tosha kwa kocha anayeng’atuka, Jupp Heynckes na kumpisha yule wa zamani wa Barcelona, Joseph ‘Pep’ Guardiola.
Kiu ya Bayern kutwaa kombe ilizidi mwaka jana, baada ya kunyang’aywa tonge mdomoni wakiwa nyumbani kwao Munich, pale Chelsea waliokuwa chini ya Roberto Di Matteo kuwafunga kwa matuta.
Aliyekosa bao muhimu mwaka jana, Arjen Robben, ndiye ameibuka shujaa wikiendi hii, kwa kufunga bao la pili na la ushindi dakika ya 89 dhidi ya timu mwenza ya Ujerumani, Borussia Dortmund, katika mechi iliyochezwa kwenye dimba la Wembley jijini London.
Wataalamu hao wa soka wa Bavaria ambao pia ni mabingwa wa Ujerumani, walitangulia kupata bao katika dakika ya 60 kupitia kwa Mario Mandzukic, mpishi wa bao hilo akiwa Robben aliyezama ndani ya 18 na kumzidi maarifa kipa Weidenfeller na walinzi wake wakashindwa kuokoa hatari.
Hata hivyo, Dortmund wanaofundishwa na Jurgen Klopp walibaki mpirani kwa dhati, na dakika nane tu baadaye walisawazisha kwa penati kupitia kwa Ilkay Gundogan, baada ya beki Dante kumchezea vibaya Marco Reus kwa kumrushia teke tumboni akiwa ndani ya eneo la hatari.
Kwa ujumla Bayern walitawala mchezo, na mabeki wa Dortmund walikuwa wakijisahau mara kadhaa na kumpa wakati mgumu kipa wao,. ndiyo maana mara mbili akashindwa kuhimili vishindo vya watu waliokuwa wamedhamiria kukamilisha msimu kiaina.
Kocha Klopp aliendelea na mfumo wake wa kawaida dimbani, licha ya kutokuwapo Mario Gotze, kwa kumchezesha Kevin Großkreutz kwenye wingi na kumhamishia Reus ndani. Maoni ya wataalamu wengine yalikuwa aanze Sebastian Kehl halafu Gündogan apande mbele zaidi, lakini Klopp hakupenda hivyo. Nyota wa Bayern, Bastian Schweinsteiger aliyeelezwa kuwa majeruhi alicheza kwa mshangao wa wengi na kufanya vyema.
Katika mechi iliyohudhuriwa na watu 86,298, akiwamo Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ambaye haikujulikana angeshabikia timu gani, Robert Lewandowski alikuwa mtulivu, pengine kwa kubanwa kijanja na watu wa Bayern, lakini wakati fulani alikwamisha mpira kimiani, licha ya kuwa kipenga kilishalia, kutokana na kutuliza mpira gambani akisaidiwa na mkono wake.
Robben alielekea kutoamini kama amewapa kombe Bayern kwa bao lake, kutokana na alivyokuwa akichagizwa na wengi kabla, hasa baada ya kuwaharibia Munich kwenye michuano iliyopita, na pia kukosa bao katika mashuti yake 24 kwenye mechi fainali tatu zilizopita.
Lewandowski alielekea kuikimbia kazi ya kupiga penati Jumamosi hii, kwa sababu alikosa moja dhidi ya Bayern hivi karibuni, akaogopa kujirudia, lakini Gundogan alijiamini, akauchukua mpira na kumpeleka sokoni golikipa Neuer, mwenyewe akiutundika mpira kwenye kamba.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

30 TWIGA STARS WAITWA KAMBINI

TAIFA STARS KWENDA ADDIS ABABA LEO