*Italia washinda 2-1
Mario Balotelli amewaliza England katika mechi kali ambapo Italia wameshinda kwa mabao 2-1, ikiwa ni ya kwanza kwa timu hizo katika fainali hizi.
Italia walianza kucheka kwa bao la mapema la Claudio Marchisio dakika ya 35 lakini Daniel sturridge akajibu kwa kusawazisha dakika mbili tu baadaye.
Katika mechi ambayo timu zilionekana kukamiana na England wangefurahi kuambulia sare, walionekana kuwa na upungufu kwenye ulinzi.
Mshambuliaji makeke na mtundu, Balotelli alimaliza kazi ya Italia kwa kufunga katika dakika ya 50 huku jitihada nyingine zote za England zikishindwa kuzaa matunda.
Mchezaji nyota wa England ambaye hajapata kufunga bao kwenye fainali za Kombe la Dunia, Wayne Rooney alipoteza nafasi nzuri na kushindwa kutengeneza nyingine, akiendeleza mkosi wake wa kushindwa kucheka na nyavu.
England wamejiweka katika nafasi ngumu ya kufuzu ambapo watatakiwa kutumia akili kwenye mechi mbili zilizobaki dhidi ya Uruguay ambao walifungwa na Costa Rica Jumamosi hii.
Uruguay hawakumtumia Luis Suarez mapema, ikielekea ni makusudi kwa ajili ya kuhakikisha anakuwa fiti baada ya majeraha yake ilia je kukabiliana na vijana wa Roy Hodgson.
Wachezaji wa England walionekana wazi kuchoka kuelekea mwisho wa mchezo, na watasingizia hali ya joto ambayo hawajazoea katika eneo la kitropiki la Manaus kama walivyodai tangu awali.
Daktari wa England, Gary Lewin katika tukio jingine la kushangaza aliumia mguu na kutolewa nje kwa machela wakati akishangilia bao la Sturridge.
Chipukizi wa Liverpool, Raheem Sterling aliyeanza dimbani alichangia kwa kiasi kikubwa kwenye timu kwa kucheza kwa kasi kwenye mashambulizi lakini England walipofika karibu na goli hawakufurukuta.
Italia wanawaliza England kwa mara nyingine, ambapo wachezaji wake Antonio Candreva na Andrea Pirlo walicheza vyema, ikiwa vigumu kujua kama kiungo Pirlo ana umri wa miaka 35 kwa kasi yake.
Kipa namba moja wa Italia, Gianluigi Buffon aliumia kabla ya mechi na hakucheza, nafasi yake ikachukuliwa na Salvatore Sirigu.
Italia wameweka rekodi ya kufunga bao katika mechi zao 15 mfululizo zilizopita za Kombe la Dunia, rekodi ambayo hakuna timu nyingine iliyopata kuweka.
Comments
Loading…