Njia gani itahitimisha msimu?
Kuna sintofahamu kubwa juu ya njia ipi itatumika kwa ajili ya kumaliza msimu wa soka 2019/2020 nchini England, baada ya Ligi Kuu (EPL) na Ligi ya Soka England (EFL) kukatishwa kwa sababu ya balaa la virusi vya corona.
Wakati mechi za ligi zimesogezwa mbele hadi Aprili 4, bado kuna wasiwasi iwapo mechi zitaweza kufanyika, kutokana na kusambaa kwa kasi kwa virusi hivyo na tayari kuna kocha na mchezaji waliokwisha ambukizwa kama si zaidi ya hao wawili.
Wakati Mikel Arteta wa Arsenal aliambukizwa virusi hivyo na wachezaji kutakiwa kuwa mbali naye kwa wiki mbili, Chelsea nao wamefunga sehemu ya mazoezi baada ya mchezaji wao, Calum Hudson Odoi kuambukizwa, na cha kushangaza majuzi ameonekana kwenye mikusanyiko ya soka la mtaani, akakanywa na wakuu wa Stamford Bridge.
Yapo maelezo kwamba serikali inataka kuzuia mikusanyiko ya zaidi ya watu 1,000, ambapo ni kwa msingi huo EPL na EFL walikuwa wakifikiria mechi zilizobaki zichezwe bila watazamaji. Hata hivyo, bado hakuna suluhisho kwa sababu miongoni mwa wachezaji na makocha wapo wagonjwa.
Kuna ushauri kwamba msimamo wa sasa wa ligi uchukuliwe kama ndio msimamo wa mwisho, mabingwa watangazwe na wa kushuka daraja kadhalika, lakini hiyo itasababisha mvutano na hata hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya EPL, jambo linaloweza kuja kugharimu sana.
Kwanza si timu zote zimecheza mechi sawa, lakini pia kuna zilizomo kwenye ukingo wa kushuka daraja kama zikishinda mechi moja tu zinajiondoa humo, na moja ya hizo ni Aston Villa ambao wana mchezo mmoja mkononi zaidi ya washindani wao walio kwenye eneo tete la kushuka daraja.
Lakini pia huko kwenye Ligi Daraja la Kwanza, kuna timu ambazo zinataka kufuzu kwa ajili ya kupanda EPL ikiwa zitashinda mechi chache zilizobaki, hivyo watachukua hatua pia. Kuna timu kama Sheffield United wanaotaka nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya, hivyo kukatiza hapa walipofika wataona hawajatendewa haki.
Njia nyingine ya kumaliza msimu huu ni kutengua matokeo yote ya mechi zilizochezwa, na timu zirudi kucheza katika mashindano walimokuwa msimu huu; jambo ambalo halitapokewa vyema na Liverpool ambao wamesubiri miaka 30 kuupata ubingwa ambao sasa ni wateule wake, na bila shaka watachukua sheria kudai kile wanachodhani ni haki yao.
Zipo timu kadhaa kwenye EPL zinaona kwamba hii ni njia nzuri, ili hali ibaki sawa kwa kila timu; wakiwa na mechi sifuri na alama sifuri wote, wasubiri kuanza msimu ujao baada ya majira ya joto na usajili mkubwa.
Maoni mengine ni kuhamisha mechi za sasa zichezwe majira ya kiangazi wakati ambao ungekuwa wa mapumziko na kupisha usajili. Hii inawezekana, hasa ikizingatiwa kwamba Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) linafikria kufuta michuano ya Euro 2020 yaliyopangwa kufanyika kiangazi cha mwaka huu.
Hii inaweza kukanganya pia, kwa sababu kuna mechi za awali za kufuzu kwa ajili ya mashindano ya Ulaya ambazo kwa kawaida huchezwa kipindi hicho, ikimaanisha itabidi kuwasiliana na Uefa ili kuona kwamba mechi hizo nazo zinabadilishwa au kusogezwa mbele. Itamaanisha pia kwamba kusogezwa mbele kutasababisha matatizo kwenye ratiba nyingine zilizo mbele.
Kucheza wakati huo mechi za kumalizia ligi ni tatizo pia, kwani wachezaji watakosa muda wa kutosha wa kupumzika kabla ya msimu mpya. Wachezaji wana haki ya likizo ya wiki tano kila msimu, wiki tatu zikitakiwa kuwa mfululizo. Wakichezeshwa mfululizo itamaanisha kwamba watachoka (burnout) mapema na kushindwa kutimiza wajibu wao vyema.
Mikataba ya wachezaji pia kimsingi humalizika mwisho wa Juni, ikimaanisha kwamba upo uwezekano kwa baadhi ya timu kukosa huduma au kuwapo mkanganyiko miongoni mwao. Wachezaji wanaweza, kwa mfano, kukosa bonasi walizoahidiwa kwenye mikataba iwapo wamefanya kazi iwapasayo kuzipata baada ya muda kumalizika.
Hata hivyo, kuna jambo lililo nje ya uwezo wa watu wote – kwamba maafa haya ya virusi vya corona bado hayajulikani yatamalizika lini; yanaweza kuendelea hata wakati huo wa kiangazi na mbele yake zaidi. Hakuna uhakika kwamba wakati huo hali itakuwa nzuri na hivyo rahisi zaidi kucheza kuliko sasa.
Upo ushauri kwamba zichezwe mechi moja moja miongoni mwa wanaokaribiana sana ili kuamua nani acheze Ulaya msimu ujao na pia kuamua wa kushuka daraja. Hata hivyo hata njia hii inaweza kusababisha mvutano mkubwa miongoni mwa timu zitakazoona hazitendewi haki