WADAU mbalimbali wameendelea kukosolewa na wadau mbalimbali kwa mpangilio wake wa bajeti ya mwaka huu ambao umeiacha kando sekta ya michezo.
Wakizungumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati tofauti katika mahojiano maalum walisema kuwa serikali mwaka huu ilizindua uwanja wa kisasa wa michezo uliogharimu shilingi zaidi ya bilioni 50 kwa ujenzi wake, lakini imejikita zaidi katika makusanyo badala ya kuangalia jinsi gani ya kuendeleza michezo hiyo.
Mwananchi Jumapili, imebaini kuwa mwaka 2008/2009, Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo iliingizia serikali Shilingi milioni313.5 kutoka vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mapato ya mechi zikiwamo za ligi kuu.
Wadau hao wanaishangaa serikali kwa uamuzi wake wa kisogo michezo, sekta ambayo imekuwa ikipigiwa kelele na kupewa kipaumbele na Rais Jakaya Kikwete.
Wanahoji kitendo cha Kikwete kuruhusu ajira kwa makocha wa michezo, akiwamo kocha wa timu ya soka ya taifa, Marcio Maximo ambaye analipwa mshahara na serikali.
Lakini, wanaishangaza serikali hiyo hiyo kutoizungumzia lolote michezo kama chanzo cha mapato na mchango, matarajio ya michezo kwa Pato la Ndani la Taifa (GDP).
Mmoja wa wadau hao, anahisi kuwa hilo linachangia kurudisha juhudi za wadau wengine wanaochangia kukuza kiwango cha michezo.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili unaonyesha kuwa mwaka jana, serikali ilitenga Shilingi 21,165,185,000 kama bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, lakini sekta ya michezo ilipangiwa kukusanya Shilingi 313,451,000, kati ya hizo, Sh120,000,000 zikitokana na viiingilio Uwanja wa Taifa.
Mjumbe wa Heshima wa Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa, Said El Maamry alisema: “Inafadhaisha kuona bajeti ya mwaka huu imeipa kisogo michezo.
“Uamuzi huu unatunyong’onyeza sana juhudi za wadau kukuza michezo, zinarudishwa nyuma badala ya kuungwa mkono nchi za wenzetu wanatukoga zinapofanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa, sisi tutaendelea kuwa wasindikizaji.
“Angali soka limepata wadhamini wengi tofauti na michezo mingine hii yote tunajua kwa vile Rais Kikwete katia mkono wake ndio maana na wadhamini wamemiminika, lakini wadhamini hao wanakatishwa tamaa na serikali pale inapoona bajeti ya serikali haina chochote wanavunjika moyo,” alisema El Maamry.
Wakati El Maamry ambaye pia aliwahi kukiongoza Chama cha Soka Tanzania ‘FAT’ sasa TFF na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), akisema hayo, mwanamichezo mwingine, Shyrose Bhanji anaeleza masitiko kwa serikali kutokana na uamuzi huo.
Bhanji, ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) alisema: “Inasikitisha serikali kuipa kisogo michezo wakati Tanzania ipo nyuma kwenye sekta hiyo.
“Haiwezekani serikali ikaachia wadau peke yao ndio waendeshe michezo, tutaendelea kuwa nyuma siku zote.
“Kama sisi (netiboli) tuna mashindano makubwa ya kimataifa yanakuja, lakini mpaka sasa hatuna sapoti yoyote ya serikali, kwa ujumla sekta ya michezo haipewi kipaumbele na serikali na ndio maana wameiacha kwa wadau ndio waishikilie.
Hata huo mpira wa miguu, wenyewe ni baada ya Rais Kikwete kuingiza mkono wake ndio tunaona na wadhamini wengine wanaelekeza nguvu zao huko…..Wangeijali michezo kwa kutenga fungu na kusapoti kila mchezo hata wadau pia wangeijali michezo yote na si kuegemea kwenye mchezo mmoja,” alisema Shyrose.
Bhanji, pia ni ofisa wa benki ya NMB ambayo imewekeza zaidi ya Shilingi milioni 700 kwenye timu ya Taifa, Taifa Stars.
Naye mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Licky Abdallah ‘Dk Licky’, yeye aliikingia kifua serikali na kueleza kuwa kosa kubwa la michezo kupewa kisogo na serikali linatoka kwa wasimamizi wa vyama vya michezo wenyewe ambao hawaiuzi michezo yao kwa wadhamini.
“Huu ni wakati mgumu kiuchumi ni wakati wa kufunga mkanda, tutaendelea kuwa nyuma kimichezo kama tutaendelea kuitegemea serikali badala ya kusaka wadhamini ili watangaze bidhaa zao kupitia michezo.
“Saudi Arabia ina makampuni yanayomwaga fedha nyingi kwenye michezo kwa sababu vyama vya michezo huko vinajiuza watoke maofisini wasake wadhamini watangaze biashara zao, migogoro, ubabaishaji ndio unaofanya hadi wafadhili washindwe kuingiza fedha zao kwenye michezo.
“Ni wakati sasa wa kubadilika na kujiuza na si kusubiri bajeti ya serikali kwani kwa kufanya hivyo tutaua michezo yote, ” alisema Dk. Licky
Comments
Loading…