in , , ,

BABA YAKE KELVIN JOHN KARIBU KWENYE KIKOMBE CHA KAHAWA

Vingi vizuri vimepita lakini havikufika sehemu ambayo vilitakiwa kufika na ndiyo maana wengi husema utajiri mkubwa upo makaburini.

Watu wanakufa na mawazo yao makubwa ambayo walishindwa kuyafikia wakiwa duniani kwa sababu ya mazingira magumu ambayo yalisababisha kutofikia sehemu waliyoota.

Hii ni dhambi kubwa sana, dhambi ambayo hukumu yake ni najuto kwa wale ambao unawaacha hai.

Wengi tunajutia kipaji cha Haruna Moshi “Bobani” kwa sababu ya dhambi yake aliyowahi kuifanya ya kutocheza soka la kulipwa.

Mioyo yetu inaumia, nafsi zetu zinamanung’uniko makubwa sana kwa sababu tuliona kipaji cha Haruna Moshi “Bobani” kilitakiwa kufika mbali tofauti na kilipoishia.

Imebaki stori tu ambayo tunaisimulia kuwa aliwahi kutokea Haruna Moshi “Bobani” ila kwa sababu ya kukosa wasimamizi wazuri na yeye binafsi kutojitambua hakuweza kufika mbali katika maisha yake ya soka.

Kitabu chetu cha soka kitabaki kumkumbuka tu kama mtu aliyetumia muda mwingi kutufurahisha katika uwanja wa zamani wa taifa kwa sasa “Uwanja wa uhuru”.

Uwanja ambao ulimnyima uhuru wa kuwaza mbali, uwanja ambao ulimnyima uhuru wa kutamani kutajirika kupitia mpira na ndiyo uwanja ambao ƴulimpa uhuru wa kukuza kichwa kila alipokuwa anashangiliwa na mashabiki waliokuwa jukwaani.

Akili yake haikuwaza nini maana ya yale makofi, alikosea kwenye mapokeo ya makofi yale yaliyokuwa yanatoka jukwaani.

Wakati unakunywa fundo la kahawa niliyokuandalia natakiwa kukumbusha umkunbushe mwanao Kelvin John kuwa makofi anayopigiwa kwa sasa anatakiwa kuyachukulia kama deni kubwa ambalo anatakiwa kulilipa kwa kutumia miguu yake.

Hatakiwi kujiona kama kafika, hiyo ni hatua ya kwanza kati ya hatua 99 anazotakiwa kupiga ili kufikia mafanikio.

Nilitamani kwenye kahawa hii niliyokuandalia , Kelvin John angekuwepo nimwambie kuwa makofi yale ni ishara ya wewe kufukuzwa nchini.

Hutakiwi kuwepo hapa Tanzania, hutakiwi kuvimba kichwa kwa sababu ya makofi ya mashabiki hawa wasiokuwa na huruma na kipaji chako.

Mashabiki ambao leo wanaweza kukusifia kesho wakakutukana. Lakini kwa sababu wewe ni baba yake najua ukimwambia neno lako litakuwa zito kuzidi mimi.

Moyo wangu unaogopa kuumia tena kama ulivyoumia kipindi cha Mrisho Ngasa.

Alikosa washauri wazuri na inawezekana mzazi wake alichangia Mrisho Ngassa kutofika sehemu kubwa, amekuja kushtuka kuwa anatakiwa kuwa sehemu kubwa umri ulikuwa umeenda ikawa ngumu kwake kufanya chochote kikubwa kama ambavyo alivyokuwa na umri mdogo.

Huu ndiyo muda sahihi kwa Kelvin John kuandaliwa mazingira mazuri ya kumwezesha kucheza soka la kulipwa.

Ndiyo muda sahihi wa kumwandalia wasimamizi bora wa kipaji chake. Wasimamizi ambao watamuongoza vyema.

Wasimamizi ambao watamshauri kuhusu maendeleo ya kipaji chake. Kipi akifanye ili kipaji chake kiwe bora.

Muda wa mazoezi yake binafsi auzingatie, afikirie kuimarisha miguu yake na akili yake kuliko kitu chochote.

Awe na njaa ya mafanikio, njaa ambao itamfanya asijaribu kujiingiza kwenye tabia ambazo zitaatarisha kipaji chake.

Najua kuna watu wengi watakuja kwako kama mzazi na karatasi ndefu ambazo zitakupa uvivu kusoma huku mezani wakiwa wameweka Milioni 15.

Akili zao zinaamini ni ngumu kwako kukataa pesa hizo ili kumruhusu mwanao acheze hapa Tanzania.

Mpira wetu hauna shukurani mzee wangu, leo watamsajili Kelvin John kwenye timu yao ila kesho watamletea mshambuliaji kutoka nje apambane naye.

Hawajali kipaji cha mchezaji mchanga, wanachofikiria wao ni leo, neno kesho halipo katika akili zao.

Ndiyo maana nimekuita kwenye meza hii ya kahawa nikukumbushe kuwa mpira ndiyo uliomfanya Cristiano Ronaldo awe tajiri ilihali alitoka kwenye familia ya kimasikini.

Leo hii wazazi wake wanafurahia matunda ya kipaji ch a mwano kwa sababu walimpatia watu sahihi wa kusimamia kipaji chake.

Leo hii baba yake Neymar ni tajiri kwa sababu aliamua kuwekeza biashara kwenye miguu ya mwanae.

Haina haja ya kufungua duka la kina Mangi wakati miguu ya mwanao Kelvin ni biashara kubwa sana ambao itakupa heshima kubwa sana.

Muda huu wewe unatakiwa kuwa mshauri wa kwanza wa Kelvin. Mpe ushauri ambao utamjenga kufikia sehemu ambapo Mbwana Samatta hajafikia.

Mjenge kuwa mtu mwenye njaa ya mafanikio, mtu asiyeridhika na mafanikio madogo, mtu ambaye kila hatua anayopiga aone siyo mwisho wa safari yake na hivi vyote ataweza kuvifikia kama vazi nidhamu atalivaa kila sekunde ya maisha yake.

Vazi nidhamu litamfanya awe anamuomba Mungu. Vazi nidhamu litamfanya awe na hofu ya neno kesho.

Litamfanya kuona mazoezi na kusikiliza wakufunzi wake pamoja na kuwaheshimu watu wote kuwa ni ngazi ya kumpeleka kwenye kilele cha mafanikio ya kipaji chake.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

TUZO MCHEZAJI BORA ULAYA

Tanzania Sports

YANGA NA MTIBWA, KONDOO ALIYETOKA USINGIZINI NA KONDOO ALIYE MALISHONI