in , ,

Baada ya kumfukuza Dismass Ten mashabiki wameongezeka uwanjani ?

Dismas Ten

Umelisoma vizuri swali langu? umetafakari majibu yake? rudia tena kulisoma swali langu vizuri. Swali ambalo binafsi mimi limekuwa likinisumbua sana akili yangu.

Yanga walitaka kutuaminisha kuwa Dismass Ten alikuwa chanzo cha mashabiki wa Yanga kutohudhulia uwanjani kwa sababu tu hakuwa na mdomo.

Hakuwa na mdomo wa kuwafanya mashabiki watoke majumbani kwao na kwenda mpaka uwanja wa Taifa kwa ajili ya kuitazama na kuishangalia timu yao pendwa ya Yanga.

Wakaingia rasmi kucheza muziki huu, muziki wa kutomtaka Dismass Ten, muziki wa kutaka kuwa na mtu mwenye mdomo haswaa kama ilivyokuwa kwa Jerry Muro.

Kwao wao Jerry Muro ulikuwa mfano wa kumwadhibu Dismass Ten. Aliadhibiwa haswaa. Walitoa mifano mingi sana. Enzi za Jerry Muro watu walikuwa wanakuja uwanjani.

Enzi za Jerry Muro mashabiki wa Simba walikuwa wanyonge haswaa. Ndizo enzi ambazo waliitwa wa mchangani, ndizo enzi ambazo mashabiki wa Simba walikuwa hawana nguvu mbele ya mdomo wa Jerry Muro.

Hiki ndicho mashabiki wa Yanga walichokuwa wamekikosa kipindi ambacho Dismass Ten yupo na Yanga. Walikosa kuona mtu anayewazodoa mashabiki wa Simba.

Walikosa mtu ambaye angesimama kifua mbele na kujimwambafai kuhusu Yanga. Na kwa bahati mbaya zaidi Dismass Ten alikuwa kipindi ambacho Haji Manara alikuwepo kama msemaji wa Simba.

Haji Manara ambaye alikuwa na mdomo haswaa, Haji Manara ambaye alikuwa anawanyanyasa haswaa mashabiki wa Yanga. Huu ndiyo ukawa mtihani kwa Dismass Ten.

Alitakiwa ashindane na mdomo wa Haji Manara. Alitakiwa arudishe kila mshale uliokuwa unarushwa na Haji Manara kumwelekea yeye. Kwamba Mnyakusya amzidi Mzaramo kuongea.

Dismass Ten alijua udhaifu wake, hakuwa mwepesi mdomoni, Ila alikuwa mwepesi kwenye kichwa chake. Alikuwa mbunifu mzuri sana. Alijitahidi sana kufikiria vitu vya kuboresha kwenye idara yake ya habari.

Alileta Yanga TV ambayo haikuwepo awali, akaweka mpangilio mzuri kwenye kipindi cha Yanga kikawa kinavutia haswaa kutazamika mwanzo hadi mwisho.

Akaleta jarida la Yanga, Moja ya jarida bora sana kuwahi kutokea kwenye vilabu vyetu hapa nchini, lilikuwa na mpangilio mzuri kuanzia rangi, picha na habari zilizokuwemo ndani.

Pale makao makuu ya Yanga alitengeneza ofisi maalumu ya kufanyia mikutano na waandishi wa habari. Ofisi ambayo ilikuwa bora sana na yenye kuvutia, na kwenye kipindi chake mitandao ya kijamii ilikuwa inaendeshwa vyema.

Alijua udhaifu wake uko wapi na alijua hawezi kulazimisha kuwa muongeaji. Unaikumbuka hadithi ya Musa? Musa ambaye alikuwa anajaribu kukwepa maagizo ya Mungu kisa hakuwa anajua kuongea?

Mungu alijua kilichokuwemo kichwani mwa Musa kuliko kilichokuwemo Mdomoni mwake, ndiyo maana akamwambia nitakupa Haruni awe anaongea mbele ya wana wa Israel kile ulichokuwa nacho kichwani .

Kichwani kwa Musa kulikuwa na maono, kichwani kwa Dismass Ten kulikuwa na ubunifu, ubunifu ambao aliuonesha kwa kiasi kikubwa Lakini mdomoni hakukuwa na kitu na watu walitaka kilichokuwepo mdomoni mwake na siyo kichwani mwake.

Walitaka afanye kazi kama Jerry Muro au Haji Manara huku wakisahau kuwa wakati Jerry Muro yupo timu ilikuwa inafanya vizuri sana ndiyo maana mashabiki walikuwa wanaenda uwanjani.

Hata kipindi cha Haji Manara, Simba inafanya vyema sana ndiyo maana mashabiki wanaenda uwanjani mara kwa mara.

Turudi kwenye swali letu la awali . Dismass Ten hayupo tena ila kuna Antonio Nugaz ambaye ndiye mwenye mdomo wa kuwaita mashabiki uwanjani na Hassan Bumbuli kama Afisa Habari wa Yanga. Tujiulize mashabiki wanaenda kwa wingi uwanjani?

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Liverpool watapindua meza Madrid?

Top 10 most-watched YouTube goals featuring Lionel Messi, David Beckham and other legends