Kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya England, Mohamed Salah ana uwiano wa bao katika kila dakika 86 za EPL. Yeye ndiye mwenye uwiano mzuri zaidi akifuatiwa na Sergio Aguero anayeshikilia uwiano wa bao moja katika kila dakika 94. Wa tatu ni Charlie Austin wa Southampton. Ana bao moja kwenye kila dakika 100. Ni hawa watatu pekee wanaomzidi Pierre-Emerick Aubameyang kwenye kipengele hiki cha takwimu.
Uwiano wa bao kwenye kila dakika 102 za michezo ya EPL unamuweka mshambuliaji huyo wa Arsenal kwenye nafasi ya nne. Anamuacha nyuma Harry Kane anayeshika nafasi ya tano akiwa na uwiano wa bao katika kila dakika 106 za mchezo. Ndio, anamzidi Harry Kane. Huu ni mwanzo mzuri sana kwa mshambuliaji ambaye ndio kwanza anaanza kuyazoea maisha ya kwenye EPL.
Msimu wa Arsenal wa Ligi Kuu ya England unaonekana umekwishapotea. Washika bunduki wanacheza michezo yao ya nyumbani Emirates wakitazamwa na siti nyingi mno zilizo tupu. Washabiki wamepoteza shauku ya kuitazama timu yao kwenye Ligi Kuu ya England. Lakini Aubameyang hasumbuliwi na jambo hili. Anafanya vizuri mno. Aliweka moja wavuni kwenye ushindi wa 3-2 dhidi ya Southampton Jumapili.
Mshambuliaji huyu wa zamani wa Borussia Dortmund amefunga kwenye kila mchezo kati ya minne ya karibuni aliyoichezea Arsenal kwenye EPL, na akavunja rekodi pia kwenye mchezo dhidi ya Southampton. Akiwa na jumla ya mabao sita na pasi moja ya bao mbaka sasa kwenye EPL, anakuwa amehusika moja kwa moja na mabao mengi zaidi kuliko mchezaji yeyote kwenye michezo saba ya kwanza ya EPL akiwa na klabu ya Arsenal.
Inafahamika kuwa Arsene Wenger amehamishia nguvu na umakini wake wote kwenye Europa League. Hii si tu nafasi pekee ya Arsenal ya kushinda taji msimu huu ila pia ni nafasi yao ya maana zaidi ya kurejea kwenye Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Aubameyang hana uhalali wa kucheza Europa League na hili limemnyima nafasi kung’ara zaidi akiwa na uzi wa Arsenal msimu huu.
Hata hivyo kiwango chake kinawapa Arsenal matumaini makubwa. Uwiano wake wa bao moja katika kila dakika 102 ni rekodi inayomfanya kuketi miongoni mwa washambuliaji bora zaidi wa EPL kwa sasa. Kumpiku Harry Kane aliyeshinda kiatu cha dhahabu cha EPL msimu uliopita kunamfanya astahili kiwango cha kupendeza cha sifa.
Inaweza kusemwa kuwa uwiano huu mzuri wa mabao si kitu kwa kuwa hata Olivier Giroud aliyeihama Arsenal Januari alisifika kwa uwiano mzuri wa mabao na jambo hilo bado halikuweza kuwapaisha Arsenal kokote. Lakini ikumbukwe, kasi ya ajabu ya Aubameyang inamuweka mahala tofauti kabisa na Giroud. Namna alivyoiwahi pasi ya Danny Welbeck Jumapili na kuisawazishia bao klabu yake ni ushahidi wa wazi. Mshambuliaji huyu ana uwezo wa ajabu wa kukimbia kwa kasi na kuifungulia timu yake mianya ya kutengeneneza nafasi nzuri za mabao.
Takwimu zinaonesha kuwa nwanasoka huyu bora wa Afrika wa 2015 ndiye mchezaji wa Arsenal aliyekimbia kwa kasi zaidi kwenye kila mchezo kati ya minne ya karibuni ya timu hiyo. Aliweza kuifikia kasi ya kilomita 35.3 kwa saa. Anaonesha dhahiri kuwa yuko kwenye kiwango bora cha kutosha kutumainiwa na Washika bunduki hawa wa London.
Ameongeza kitu kikubwa kwenye safu ya mashambulizi ya Arsenal. Baadhi wanamtazama kama mbadala wa Lacazette aliyejiunga na Arsenal kwenye majira ya joto mwaka jana. Lakini badala yake uwepo wake unaweza kumuinua Mfaransa huyo. Aubameyang anaweza kushirikiana vyema na Lacazette ama Welbeck na kupeleka balaa langoni mwa wapinzani.
Wachezaji wa Arsenal na Arsene Wenger wanahamasika mno na kiwango cha Aubameyang. Rekodi anazoanza kuziweka zinampa na yeye mwenyewe hali ya kujiamini. Hakuna cha zaidi cha maana anachoweza kuifanyia Arsenal msimu huu hata hivyo. Kipimo cha kweli kitakuja msimu ujao. Lakini kuna faida kubwa kwa yeye na timu yake inayoletwa na kiwango cha sasa cha nyota huyo. Ni dalili nzuri kwa Arsenal kuelekea msimu ujao.