Siku moja baada ya pazia la Ligi Kuu ya England (EPL) kushushwa, imetangazwa kwamba klabu ya Aston Villa inauzwa.
Aston Villa imenusurika kushuka daraja msimu huu na msimu uliopita chini ya Kocha Paul Lambert ambaye majuzi alikaririwa akisema alikuwa hajui hatima yake.
Mmiliki wa klabu hiyo, Randy Lerner ameona hakuja tija kuendelea kuimiliki na ametangaza Jumatatu hii kwamba anaipiga mnada.
Mmarekani huyo alipata umiliki kamili wa Villa mwaka 2006 baada ya bodi kukubali dau lake la pauni milioni 62.6 lakini sasa inaelezwa kwamba ameamua kutafuta mtu wa kuinunua. Timu yao imemaliza ikiwa nafasi ya 15 msimu huu, pointi tano tu juu ya eneo la hatari la kushuka daraja.
Klabu hiyo inayojulikana pia kwa majina ya Villa, The Villa, The Villans na The Lions ipo maeneo ya Witton, jijini Birmingham, moja ya majiji matatu makubwa ya England. Mengine ni Manchester na Liverpool. Klabu ilianzishwa 1874 na wamekuwa wakichezea uwanja wao wa sasa wa Villa Park tangu 1897.
Villa ni waasisi wenza wa Ligi ya Soka 1888 na pia waasisi wenza wa EPL 1992 ambamo wamebaki bila kushuka tangu wakati huo. Hii ni moja ya klabu kongwe na zenye mafanikio zaid katika soka ya England, ikiwa nafasi ya nne kwa kupata mataji zaidi nchini England.
Villa walitwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza mara saba, Kombe la FA mara saba, Kombe la Ligi mara tano na Super Cup ya Uefa mara moja. Walitwaa pia Kombe la Ulaya 1981/82, hivyo ni moja kati ya timu tano za England zilizopata kutwaa kombe ambalo sasa linajulikana kuwa la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, hawajapata kutwaa kombe lolote tangu 1996. Wapinzani wao wa jadi ni Birmingham City wanaotoka jiji moja.