Miongoni mwa vitu ambavyo wakazi wa jiji la Arusha wanajutia hivi leo ni kufa kwa mbio maarufu za Mount Meru International Marathon.
Ni ukweli usiopingika mbio hizi zilikuwa maarufu kuliko hata zile zinazofanyika katika mji jirani wa Moshi za Kilimanjaro Marathon.
Mbio za Mount Meru International Marathon zilijijengea umaarufu kiasi hata cha kuingizwa katika kalenda ya shirikisho la mbio za marathon duniani yaani Association of International Marathons AIMS.
Watanzania wachache wanaweza kuamini kuwa mbio hizo ziliweza kuvutia viongozi kadhaa wa AIMS akiwemo hata Rais wake Ndugu Chosa tajiri toka Japan kuhudhuria mara kadhaa kila wakati zikiendeshwa hapo mjini Arusha.
Chini ya uongozi wa Ndugu Ahmed Sharrif aliyekuwa mtumishi wa Banki Kuu Arusha na Kassim Mamboleo aliyekuwa Afisa Utamaduni mkoa waliweza kuendesha michezo hiyo mfululizo zaidi ya miaka kumi chini ya udhamini wa watengenezaji vinywaji baridi Pepsi Cola.
Kinachoshangaza ni kufa ghafla kwa michezo hiyo baada ya kustaafu kwa watendaji wakuu Sharrif na Mamboleo.
Hivi ni kweli wakazi wa Arusha na haswa ukitilia maanani kuwa Arusha ni kitovu cha riadha nchini wanashindwa kurudisha mbio hizi?
Katika utafiti wangu inasemekana mbio hizo ziliuzwa kwa mtu binafsi aitwaye Nditi na aliyekuwa afisa michezo mkoani Arusha ndugu Andrew Muneja . Ndugu Nditi ana hati miliki za mbio hizo hivyo basi yeyote anayetaka kufufua mbio hizo lazima awasiliane naye na kumlipa pesa kabla hajaendesha mashindano.
Sio vyema kuingilia masuala hayo lakini bado wakazi wa Arusha wanahitaji mbio kama hizo ili iwe sehemu ya kivutio cha utalii jijini hapo.
Mount Meru International Marathon ni mtihani mkubwa kwa Afisa Michezo mpya wa mkoa Bi Mwamvita Okeng kwani dunia nzima hivi sasa inatilia sana mkazo katika michezo na utalii.
Upende usipende tunahitaji kuona Mount Meru International Marathon inarudi ili nayo itoe changamoto kwa wanariadha wetu nchini.
Comments
Loading…