Miaka 20 imepita, miaka yenye rangi mbali ndani ya maisha ya Arsene
Wenger ndani ya kikosi cha Arsenal.
Hapana shaka rangi nyeupe ilitanda katika ngozi ya mwili wake ndani ya
miaka 10 ya kwanza.
Miaka ambayo alifanikiwa kupata mafanikio makubwa katika soka la England.
Mafanikio ambayo yalimpa heshima kubwa sana ambayo vizazi vingi vitaikumbuka.
Ndiyo miaka kumi ambayo alifanikiwa kupata kushinda makombe matatu
pekee aliyonayo ya ligi kuu ya England, kombe ambalo kwa sasa
linaonekana gumu kwake kushinda tena.
Hapana shaka nyakati hizi zenye majira ya ushindani na mapinduzi
makubwa ndani ya mpira duniani hazitoi nafasi kwake yeye kushinda tena
kombe hili.
Upinzani mkubwa umeongezeka, mapinduzi ya uwekezaji mkubwa wa timu
mbalimbali ndani ya uwanja yanafanyika kwa kiasi kikubwa ndiyo maana
siyo jambo la kushangaza Manchester City imetoka kwenye kisigino mpaka
kichwani.
Mapinduzi ambayo yanaipa nafasi Chelsea kuwa timu ambayo ina mafanikio
makubwa ndani ya miaka kumi iliyopita mbele ya Arsenal.
Mapinduzi haya hayaishii kwa kuyatazama katika matumizi makubwa pekee
ya kununua wachezaji pekee, yanaenda mbele zaidi ya hapo. Unaweza
ukanunua wachezaji kwa gharama kubwa lakini ukakosa kocha mwenye mbinu
za kisasa zinazoendana na wakati huo.
Mbinu ambazo zitatumika ndani ya uwanja na nje ya uwanja kuwaongoza
wachezaji wako.
Mbinu ambazo zitawafanya wachezaji wajiamini kila wanapoingia uwanjani.
Hii imekuwa tofaufi ndani ya kikosi cha Arsenal kwa sasa, wachezaji
hawajiamini, hawajitumi kwa ajili ya timu.
Makosa mengi binafsi yamekuwa ndani yao, safu ya ulinzi imekuwa
ikifanya makosa yale yale miaka nenda rudi.
Ile Arsenal iliyofanikiwa kumaliza ligi bila kufungwa ( Invincible) na
kwenda mechi 49 bila kupoteza mchezo wowote ndani ya ligi kuu ya
England haipo tena kwenye mikono ya Arsene Wenger.
Mikono ya Arsene Wenger imeshikilia Burnely iliyovaa vazi la Arsenal.
Mikono ambayo imetapakaa rangi nyeusi.
Rangi nyeupe haipo tena kwenye ngozi ya mwili wake kama awali, giza
limeshatanda katika maisha yake.
Hana uhakika wa kukimbia tena kwa sababu miguu yake haina nguvu, akili
yake haifikirii kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa awali.
Uwezo wa kuiongoza tena Arsenal katika mafaniko ya hali ya juu
umepungua , miaka kumi yake bora ya awali imeshapita.
Yuko ndani ya miaka kumi ambayo yuko kwenye chungu cha moto, miaka
kumi ambayo inaweza kufuta heshima yake aliyofanikiwa kuiweka ndani ya
miaka kumi iliyopita.
Historia haimbebi tena kipindi hiki kigumu anachopitia, Arsenal
haiitaji kocha wa aina yake tena ili kushindana katika mashindano
makubwa.
Damu mpya inahitajika kuinusuru Arsenal kipindi hiki kigumu walicho nacho.
Kipindi hiki Arsenal hamwihitaji tena Arsene Wenger kwa sababu kadri
muda unavyozidi kwenda anatengeneza Arsenal dhaifu.
Arsenal ambayo tangu mwaka huu uanze imepoteza michezo saba na
kuruhusu goli kwenye mechi kumi zilizopita.
Safu yake ya ulinzi siyo imara tena, haiwezi kulinda kibarua cha
Arsenal Wenger. Safu ya ushambuliaji haina nguvu za kutetea kazi ya
Arsene Wenger
Hata mbinu zake kwa sasa siyo silaha tena za kumlinda, hana silaha
yoyote ya kujitetea kwa sasa. Silaha zake zimekosa makali tena.
Hawezi kuwepo kwenye vita ya kugombania nyama aliyenona.
Kitu pekee ambacho kinaweza kumpa heshima kubwa kwa sasa ni kukubali
kuondoka kwa heshima.