*Wenger atamba, Demba Ba abisha hodi
Arsenal wamerusha makombora na kuzidi kuwafukia Reading mkiani, huku tetesi za usajili mpya zikizidi kushika kasi.
Katika mzunguko wa 17 wa Ligi Kuu ya England (EPL), Arsenal waliwacharaza Reading mabao 5-2, Arsene Wenger akisema majibu ya shutuma dhidi yake ni kwa vitendo.
Alimchezesha Theo Walcott kwenye ushambuliaji wa kati anaotaka anapojivutavuta kumwaga wino kuongeza mkataba Emirates.
Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya England alifanikiwa kupachika bao moja, la tano, wakati jingine lilifungwa na Lucas Podolski na matatu yakifungwa na kiungo Mhispania, Santi Cazorla.
Ilikuwa furaha kwa Wenger na wachezaji, kwani wamepata msukosuko kutoka kwa wadau, baada ya kuangukia pua kwa vibonde Bradford, katika mechi ya robo fainali ya Capital One Cup.
Wenger alionekana akibadilishana mawazo mara kwa mara na msaidizi wake, Steve Bould, ambaye vyombo vya habari vilidai kwamba hawaelewani.
Kwa ushindi huo, Arsenal wamepanda hadi nafasi ya tano, wakibakisha pointi mbili kuingia eneo walilozoea la ‘nne bora’.
Manchester United wanaongoza ligi kwa pointi 42, wakifuatiwa na jirani zao – Manchester City wenye pointi 36, Chelsea wakifuatia na pointi 29, lakini wana mchezo mmoja mkononi.
Arsenal wanawapumulia jirani zao wa kaskazini mwa London, Tottenham Hotspurs wanaofunzwa na Andre Villas-Boas, kwani wanatofautiana kwa pointi mbili pia.
Hata hivyo, Arsenal wanafuatwa kwa tofauti ya mabao na Everton na West Bromwich Albion, huku vijana wanaochipukia, Norwich wakifuata kwa tofauti ya pointi mbili.
Stoke hawako mbali sana, kwani wameweka kibindoni pointi 24, huku Swansea City na West Ham United wakifungana kwa pointi 23.
Liverpool waliokuwa wanalenga kupanda hadi nne bora karibuni wameanguka hadi nafasi ya 12 kwa pointi 22 baada ya kufungwa wikiendi iliyopita.
Wanafuatiwa na Fulham na Aston Villa, kila moja ikipungua pointi mbili mbili kwa mtiririko huo. Newcastle waliokosa mashiko siku hizi wanashikilia nafasi ya 15, Sunderland wa 16 na Southampton wa 17.
Katika eneo la hatari, wapo Wigan ambao kwa safari hii ni wageni kidogo, wakiungana na waliokwishazoea hapo, Queen Park Rangers (QPR) na Reading wanaobeba wenzao wote.
Akizungumza baada ya mchezo wa juzi, kiungo wa kimataifa wa Arsenal aliyerejea dimbani baada ya kuwa majeruhi kwa zaidi ya mwaka, Jack Wilshere alisema anaona Arsenal ile nzuri ya zamani inarejea.
Maneno hayo yanaungwa mkono na mchambuzi wa masuala ya soka na mchezaji wa zamani, Garry Naville, aliyesema Arsenal wanaonekana kuamka.
Hata hivyo, baada ya kufunga mabao manne kipindi cha kwanza, kipindi cha pili walijisahau na kupachikwa mabao mawili ya mfululizo, kabla ya kurejea tena kwenye hali njema.
Mabao ya Reading ambao kocha wao, Brian McDermott sasa yu katika kitimoto, yalifungwa na
Adam Le Fondre na Jimmy Kebe.
Wakati hayo yakijiri, mshambuliaji mahiri wa Newcastle, Demba Ba ameashiria kwamba anataka kujiunga na Arsenal.
Ba aliulizwa juu ya tetesi hizo, akasema hajui, bali katika mkataba wake kuna kipengele kinachomruhusu kuondoka wakati wa dirisha dogo kwa bei ya pauni milioni saba hivi.
Akasema vyombo vya habari vinaandika kwa sababu vinajua hilo, na kwamba ni juu ya Arsenal kunyanyuka na kwenda Newcastle kupeleka maombi yao, akisema ni aina ya klabu inayoelekea kutimiza ndoto zake.
Wilshere mwenyewe yu mbioni kusaini mkataba wa muda mrefu, akisema anatarajia wakamilishe mazungumzo ndani ya wiki chache zijazo. Walcott anaendelea na mazungumzo, naye alisema anatarajia mambo yatakuwa mazuri.
Comments
Loading…