*Liverpool walala kwa Manchester City
*Man United wapambana, wafuta aibu
MTOTO hakutumwa dukani kwenye minyukano ya Ligi Kuu ya England (EPL) siku ya Boxing Day.
Timu zote 20 zilishuka dimbani kutafuta ushindi muhimu ili ama ziongoze ligi, ziwe katika nne bora, ziepuke kuingia tatu za chini au kujinasua mkiani.
Waliocheka zaidi walikuwa Arsenal, kwani walitekeleza kazi yao na pia wakasaidiwa na Manchester City hivyo kurejea kwenye usukani wa ligi walikokuwa kwa muda mrefu kabla ya kuondoshwa na Liverpool.
Arsenal walipambana dhidi ya West Ham waliowang’oa Chelsea kwenye michuano ya Kombe la Ligi majuzi, na Arsenal walitangulia kufungwa.
Hata hivyo, Theo Walcott aliyetoka kwenye mapumziko ya majeraha wiki iliyopita, alifunga mabao mawili na majeruhi mwingine aliyepona pia, Lukas Podolski akafunga la tatu na kuwafurahisha washabiki.
Arsenal wakicheza ugenini walitawala kipindi cha kwanza lakini walijikuta wakiachwa nyuma kwa bao la Carlton Cole aliyefumania nyavu baada ya kipa Mpolishi
Wojciech Szczesny kutema mpira ulioonekana kumzidi nguvu.
Walcott alisawazisha kabla ya Podolski kumpasia mpira na kutundika la pili kisha Mjerumani mwenyewe akafunga la tatu.
Matokeo hayo yamewashusha West Ham hadi eneo la kushuka daraja, nafasi ya 19 kutoka ya 17 na itakuwa pigo kwa kocha Sam Allardyce ambaye msimu unamwendea kombo huku Arsene Wenger akichekelea, japo kwa hadhari.
Walcott sasa amefunga katika kila mechi aliyocheza, na hadi sasa amecheza nne.
Manchester City waliowafunga Liverpool 2-1 katika dimba la Etihad kumewapandisha hadi nafasi ya pili, wakiwashusha Liverpool hadi ya nne nyuma ya Chelsea. Arsenal wana pointi 39, City 38, Chelsea 37 na Liverpool 36.
Mabao ya Man City yalifungwa na nahodha wao, Vincent Kompany na Alvaro Negredo wakati Liverpool walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Philippe Coutinho.
Katika mechi yao dhidi ya Swansea, Chelsea walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 na kuzidi kumweka Jose Mourinho katika wakati mgumu kwani anataka kuona wachezaji wake wakifunga mabao mengi kila mechi.
Mabingwa watetezi, Manchester United walikuwa wameshaloa kwa mabao 2-0 kutoka kwa Hull lakini walipigana na kufanikiwa kuyasawazisha na kuongeza la ushindi, ngoma ikamalizika kwa 3-2.
Cardiff wakicheza nyumbani walifungwa 3-0 na Southampton, Newcastle wakawasasambua Stoke 5-1 wakati Everton wakishangazwa nyumbani kwa kufungwa na washika mkia, Sunderland kwa 1-0.
Tottenham Hotspur walio chini ya bosi mpya, Tim Sherwood waliambulia sare ya 1-1 nyumbani kwao White Hart Lane walipocheza na West Bromwich Albion waliomtimua kocha wao, Steve Clarke huku Norwich walilala nyumbani pia kwa kufungwa 2-1 na Fulham waliomfukuza kocha pia.
Kwa matokeo hayo Everton wanashika nafasi ya tano kwa pointi 34 wakifuatiwa na Newcastle (33), Man United na Spurs (31), Southampton (27), Stoke (21), Swansea na Hull (20), Aston Villa na Norwich (19), West Brom na Cardiff (17), Crystal Palace na Fulham (16) wakati mkiano wapo West Ham wenye pointi 14 na Sunderland 13.
Comments
Loading…