Matumaini ya Arsenal kutwaa ubingwa katika Ligi Kuu ya England (EPL)
msimu huu yaliyokuwa yameanza kuwa makubwa yamezidi kupotea baada ya
kupoteza mechi muhimu dhidi ya Manchester United.
Kijana mwenye umri wa miaka 18, Marcus Rashford wa United alifunga
mabao mawili wakicheza nyumbani Old Trafford, kwenye mechi
iliyomalizika kwa Man U kushinda 3-2. Arsenal walianza kwenda vibaya
kwa kufungwa na Chelsea, kabla ya kutibuliwa pia na Barcelona kwenye
mechi ya mkondo wa kwanza ya 16 bora katika Ligi ya Mabingwa Ulaya
(UCL) nyumbani Emirates; wlaifungwa 2-0.
Arsenal wanaonekana bado kujiamini, kwani kwenye mechi dhidi ya
Barcelona wiki jana, walicheza vyema lakini wakashindwa kutumia vizuri
fursa kadhaa walizopata na wangeweza kuibuka na ushindi.
Wakati wakitazamwa na wengi, shinikizo pia likiwa kwao ili waweze
kupanda na kuwakuta vinara wa ligi – Leicester na wapinzani wao wa
London Kaskazini – Tottenham Hotspur, walishindwa kuondoka walau na
pointi moja ugenini Jumapili hii.
Rashford alianzishwa na kocha Louis van Gaal dhidi ya timu ya FC
Midtjylland Alhamisi kwenye mechi ya Kombe la FA na akafunga mabao
mawili. Mchezaji wa zamani wa Man U, Danny Welbeck naye aliwazodoa
Mashetani Wekundu kwa kuwafunga tena, lakini Ander Herrera aliwafunga
Arsenal. Mesut Ozil alirejesha matumaini kwa kupachika bao lakini
United walisimama imara hadi mwisho na kushinda mechi hiyo.
Arsenal hawajatwaa ubingwa tangu 2004, na kwa matokeo ya Jumapili hii
wanabaki nafasi ya tatu wakiwa na pointi tano pungufu ya vinara na
tatu nyuma ya Spurs. Man U wamepanda hadi nafasi ya tano, wakiwa na
ushindi wa kwanza katika mechi tatu za EPL.
United walikuwa na kikosi cha vijana bila wazoefu wengi na Arsenal
walishindwa kutumia fursa hiyo kuonesha wana nia kweli ya kutwaa
ubingwa. Leicester walipata ushindi mwembamba dakika za mwisho dhidi
ya Norwich na Spurs wakawashinda Swansea ikimaanisha Arsenal wana kazi
ngumu zaidi.
Kocha Arsene Wenger ameshuhudia timu yake ikiyumba kwenye mashindano
matatu tofauti, kwani walitoshana nguvu na Hull kwenye michuano ya
Kombe la FA, hivyo kuwa na mechi moja ya ziada; kwa ajili ya marudiano
kujua iwapo wataingia robo fainali au la. Hili linaweza pia
kuwaongezea majeruhi.
Wakati kaimu nahodha msaidizi wa klabu hiyo, Per Mertesacker alisema
tatizo lao kubwa ni kwenye ushambuliaji, mambo yalikuwa tofauti
Jumapili hii na Wenger alilalamika jinsi walivyokubali mabao mawili
marahisi kufungwa. Mertesacker alikuwa benchi, nafasi yake
ikachukuliwa na Gabriel.
Mechi ijayo Arsenal watacheza na Swansea, wakati United watapepetana
na Watford walio katika nafasi ya 10.