*Angel Di Maria: Nataka kwenda PSG
*Christian Benteke anaenda Liverpool
Arsenal wanafikiria kumsajili mshambuliaji wa Manchester City, Edin Dzeko, 29, kwa ajili ya kusaidiana na Olivier Giroud.
Washika Bunduki wa London wamekuwa wakihusishwa na kumnasa mshambuliaji wa Real Madrid, Karim Benzema, lakini duru za sasa zinapasha kwamba wanafikiria kumchukua mchezaji huyo wa kimataifa wa Bosnia badala ya Benzema.
Hofu ya Wenger ni kwamba kumtegemea Giroud peke yake ni hatari kwa sababu ya Danny Welbeck kusumbuliwa na matatizo ya goti mara kwa mara.
Arsenal wapo vizuri kwenye kiungo, kwa sababu ya kupona kwa majeruhi, Theo Walcott na Alex Oxlade Chamberlain na Walcott anaweza kucheza mbele lakini pia hurejewa na majeraha mara kwa mara.
Dzeko anatakiwa na Roma lakini mwenyewe anasema kwamba angependa kubaki Ligi Kuu ya England, na hilo limeibuka katika mazungumzo baina ya viongozi wa City na Arsenal. Dzeko anaonekana kwamba si muhimu sana katika kikosi cha msimu ujao cha City, hasa baada ya kusajiliwa kwa Raheem Sterling na uwezekano wa kuwasili Etihad kwa Kevin De Bruyne.
Wenger amekuwa akitaka kupata mshambuliaji hodari kurudi zama zile zilizopita za akina Emmanuel Adebayor naNicklas Bendter. Wiki jana alizungumzia suala la Benzema lakini akasema angelipa kiasi kikubw aikiwa mchezaji ana kitu cha kipekee akilinganishwa na wengine.
Arsenal pia wamekuwa wakihusishwa na mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang, 26, anayekadiriwa kuwa na thamani ya pauni milioni 30 lakini klabu hiyo ya Ujerumani imesisitiza kwamba hauzwi.
BENTEKE AJIANDAA KWA LIVERPOOL
Mshambuliaji wa kati wa Aston Villa, Christian Benteke anatarajiwa kutua Liverpool iwapo atafuzu vipimo vya afya.
Habari zinasema kwamba klabu mbili hizo zimekubaliana dili la pauni milioni 32.5, wakati Liver wakionekana bado wanaendelea kutafuta mbadala wa Luis Suarez waliyemuuza Barcelona misimu miwili iliyopita.
Inaelezwa kwamba Liverpool wamemtuma daktari wao kurudi England kwa ajili ya vipimo vya Benteke. Daktari huyo alikuwa na klabu nchini Austria wanakoendelea na ziara kabla ya msimu mpya kuanza.
Inaelezwa kwamba Mtendaji Mkuu wa Liverpool, Ian Ayre alikutana na mwenzake wa Villa, Tom Fox mwishoni mwa wiki na kukubaliana juu ya dili hilo baada ya Liverpool kufikia kiwango cha ada kilicho kwenye mkataba wa Mbelgiji huyo. Tayari Liver wamewasajili washambuliaji Roberto Firmino kwa pauni milioni 29 kutoka Hoffenheim na Danny Ings kutoka Burnley.
ANGEL DI MARIA: NATAKA KUONDOKA
Winga wa Manchester United, Angel Di Maria amesema kwamba anataka kuondoka Old Trafford kiangazi hiki ili akajiunge na Paris St-Germain wanaomhitaji.
Di Maria, raia wa Argentina aliyeanza vibaya msimu uliopita na Man U anaona kwamba huenda akakosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza na bora akatafute maisha Ufaransa. Man United wanataka walipwe pauni milioni 52 hata hivyo, na haijulikani kama PSG watakuwa radhi kuzitoa.
Iwapo watakubali kulipa ada hiyo, United wanafikriia kumsajili mshambuliaji wa Barcelona, Pedro, kuchukua nafasi ya Di Maria. Tayari nyota huyo ameona jinsi wenzake, Robin van Persie na Radamel Falcao walivyotupiwa viraho na kocha Louis van Gaal.
TETESI NYINGINE ZA USAJILI
Newcastle wanakaribia kumsajili mshambuliaji wa Anderlecht, Aleksandar Mitrovic, 20, kwa dau la pauni milioni 13.5 pamoja na mlinzi Chancel Mbemba, pia 20, kwa pauni milioni 7.5.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho amesema si kweli kwamba anafikiria kumsajili kiungo wa Juventus, Paul Pogba, 22, na badala yake amemfananisha na Mnara wa Eiffel ulioko Ufaransa.
Mourinho amesema kila mmoja angependa kuwa na mnara huo mkubwa lakini ukweli ni kwamba hana uwezo wa kuusimika kwenye bustani ya nyumbani kwake, akimaanisha bei yake ni kubwa.
Mourinho anajiandaa kumuuza winga Juan Cuadrado aliyemsajili msimu uliopita tu, lakini anasema hatapokea chochote chini ya pauni milioni 26.1 walizolipa wakati wakimnunua Januari hii.
Kocha wa Bayern Munich, Pep Guardiola amesema atafanya kila awezalo kumbakisha kiungo wake, Mario Gotze, licha ya kutakiwa na klabu za Juventus, Liverpool na Manchester United.
Klabu ya Fenerbahce ya Uturuki waliowasajili Robin van Persie na Nani kutoka Manchester United, wanaelekea kudhamiria kujiimarisha kwani sasa wamemgeukia winga wa Tottenham Hotspur, Aaron Lennon, 28.
West Ham na Bournemouth wameingia kwenye vita ya Leicester na kujaribu kumsajili mshambuliaji wa QPR, Charlie Austin.
Stoke wanatarajia kuvunja rekodi ya kiwnago wanachotoa kwa usajili, kwani wameandaa pauni milioni 15 kwa ajili ya kumnasa winga wa Dynamo Kiev, Andriy Yarmolenko, 25.
Aston Villa wapo kwenye mazungumzo na Spurs kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wao wa kati aliyepoteza kiwango, Emmanuel Adebayor, 31, kuziba pengo la Benteke ikiwa atakwenda Liverpool.
Bosi wa West Bromwich Albion, Tony Pulis anataka kumsainisha mkataba mpya mshambuliaji wake, Saido Berahino, 21, kabla ya kuanza msimu ujao, huku kukiwa na habari kwamba Spurs wanataka kumchukua Mwingereza huyo mwenye asili ya Burundi. Bosi wa Hull, Steve Bruce amesema anafikiria hatma yake klabuni hapo kwa sababu mambo anayotaka kufanywa na wamiliki inaelekea hayatatekelezwa.