Arsenal wamemaliza muda wa usajili pasipo kusajili mchezaji yeyote tofauti na kipa, japokuwa walikuwa na fursa ya kumchukua mshambuliaji wa kati wa Paris Saint-Germain (PSG), Edinson Cavani.
Washika Bunduki wa London wanasemekana walikataa kumwaga pauni milioni 50 ili kumchukua Emirates mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay na sasa itabidi wajipange na washambuliaji waliopo.
Arsenal waliwasiliana na jamaa wa PSG juu ya mchezaji huyo nyota ambapo walielezwa waweke mezani dau la pauni milioni lakini wakakataa, wakisema hawakuwa tayari kutoa kiasi hicho cha fedha.
Katika muda wote wa dirisha la usajili la kiangazi, Arsenal walimpata mchezaji mmoja tu, kipa mkongwe wa Chelsea, Petr Cech ambaye tayari ameonesha thamani yake, kwa kurekebisha makosa kadhaa ya mabeki wake kwenye mechi za Ligi Kuu ya England.
Baadhi ya washabiki wameachwa wakiwa wamesikitika, wengine kukasirika lakini kwa ujumla hakuna aliyeshangaa sana, kwani wanaelewa jinsi viongozi wao, akiwamo kocha Arsene Wenger wanavyofanya fursa kama hii inavyojitokeza.
Arsenal wanakuwa klabu pekee miongoni mwa zile za juu katika ligi kuu tano za Ulaya kutosajili mchezaji wa ndani kwa ajili ya kikosi cha kwanza msimu huu. Walikuwa wakihusishwa na Karim Benzema lakini dili lilipokufa wakahamishiwa kwa Cavani, na Wenger alipoonekana Paris, tetesi zikawa anakwenda kumleta Cavani.
Ilivyokuwa ni kwamba Real Madrid hawakutaka kumuuza Benzema, na Mfaransa huyo mwenyewe hakuwa na mshawasha wa kuondoka wakati Arsenal hawakuwa trayari kutoa robota la fedha ili kumpata, na hivyo hali ikabaki ‘kama juzi’, hakuna mchezaji mpya.
Ndivyo pia ikawa kwa Cavani, ambaye licha ya kuelezwa kuzongwa zongwa na uwapo wa Zlatab Ibrahimovic klabuni mwake, si mtu mwenye papara ya kuondoka, PSG wenyewe walikuwa kimya wakiwasubiri Arsenal wanaojulikana kutopenda kumwaga fedha hovyo.
Taarifa zinasema kwamba Arsenal walitakiwa waanze na ofa ya pauni milioni 50 ambazo zingeweza kukubaliwa au kutakiwa kuongeza, lakini mara moja wakaamua kupuuza, hali ambayo imewaudhi washabiki, kwani wanaamini angeweza kuwasaidia kupata ushindi kwenye mechi nyingi na hata ubingwa msimu huu.
Tim Payton wa Arsenal Supporters Trust (AST) ametoa waraka wake na humo anasema: “Arsenal wapo vizuri sana kifedha kwa hiyo inasikitisha kwamba dirisha la usajili linafungwa kwa usajili wa Petr Cech tu. Arsenal wametengeneza kikosi kizuri lakini nyongeza ya mchezaji mmoja au wawili wazuri zaidi ingeimarisha kikosi na kutoa fursa ya kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 11.
“Hakuna anayesema tununue wachezaji kwa maana tu ya kununua; lakini tunataka kuona fedha zikitumiwa kuwekeza ili kuifanya klabu kuwa imara zaidi. Hili si suala linaloathiri tu dirisha moja la usajili bali linaonekana kugusa suala pana zaidi.
“Katika miaka ya karibuni Arsenal wamefanyia mageuzi makubwa akademia yake pamoja na jopo la matabibu wake. Tunaishauri bodi sasa kuanza upya mapitio juu ya mfumo wa ung’amuzi wa wachezaji na vipaji pamona na ununuzi wa wachezaji.
“Mapitio ya aina hii ni mazuri katika utawala na yanaweza kusaidia Arsenal kuja kuwa klabu kubwa zaidi. AST itafikisha suala hili mbele ya bodi. Kwa kuwa sasa dirisha limefungwa, kikosi kimebaki kama kilivyokuwa, ambacho ni imara na karibuni kimetwaa vikombe lakini walihitaji kusajili zaidi ya Cech.”
Julai 10 mwaka jana Arsenal walimsajili Alexis Sanchez na msimu mmoja kabla walimsajili kiungo Mesut Ozil. Katika ushambuliaji wa kati wanao Olivier Giroud na Theo Walcott. Danny Welbeck bado hajawa timamu kwani anasumbuliwa na goti lakini Joel Campbell aliyekuwa Villarreal kwa mkopo amerejea Emirates.
Comments
Loading…