Wachezaji wa Arsenal wanatarajiwa kuwa wa kwanza miongoni mwa klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) kukubali kukatwa mishahara kwa ajili ya janga la virusi vya corona.
Washika Bunduki wa London wamekubaliana na uongozi wao kukatwa mishahara yao wakati huu mgumu, wakiwa pia ni ambao kocha wao, Mikel Arteta alikuwa wa kwanza kuambukizwa virusi hivyo hatari vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu.
Uongozi wa Arsenal uliingia katika mazungumzo na wachezaji wao pasipo kuwatia shinikizo, wakipewa motisha ya kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) msimu unaokuja.
Wachezaji hao watakatwa kila mmoja asilimia 12.5 ya mishahara yao, lakini watarejeshewa kima hicho cha fedha ikiwa watafuzu kwa ajili ya UCL kwa msimu wa 2021/2022.
Kadhalika, watapatiwa bonasi ya £100,000 kila mmoja ikiwa watafuzu kwa mashindano hayo, lakini pia kila mmoja atabeba kitita cha £500,000 iwapo watafanikiwa kutwaa taji la mashindano hayo, na ikiwa watatwaa taji la Ligi ya Europa, watalipwa kila mmoja £100,000.
Vijana hao waliokuwa wakifundishwa kwa muda mrefu na Arsene Wenger kisha Unai Emery kwa muda mfupi, walikuwa nafasi ya tisa wakati msimu wa ligi uliposimamishwa huku wakiwa na mechi 10 mkononi kukamilisha msimu ambao haujulikani utaanza lini tena.
Wiki jana, bosi ya watendaji wa ngazi za juu walikubaliana kuachana na theluthi ya mishahara yao kwa kipindi cha miezi 12 ijayo ili kukabiliana na athari za ugonjwa huo hatari uliosababisha watu kujifungia ndani.
Majadiliano binafsi yalikuwa yakiendelea miongoni mwa uongozi na wachezaji juu ya jinsi ya kukabili changamoto hiyo kubwa. Arsenal walitangaza kwamba hawatawakata mishahara wafanyakazi wake wala kupunguza kazi yeyote.
Bodi ya EPL ilikuwa imeamua kwamba kila klabu iwakate wachezaji wake asilimia 30 ya mishahara, lakini Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA) kiliwahamasisha wachezaji kutokubaliana na bodi. Klabu kadhaa zimeamua kuwaweka kando wafanyakazi wasiokuwa wachezaji.
Taarifa ya Arsenal imesema kwamba wamiliki wa klabu hiyo – Kroenke, Sports & Entertainment, wapo nyuma ya wachezaji, wakiwaunga mkono kwa asilimia 100 katika changamoto ya wakati huu, na watakuwa pamoja siku zote.
Wameamua pia kwamba washabiki waliokuwa wamekata tiketi za mechi zilizobaki watafidiwa iwapo zitachezwa bila watazamaji au kwamba mechi hizo zitafutwa. Arsenal ni moja ya klabu zinazotoza kima kikubwa cha fedha kwa tiketi za msimu, ikimaanisha kwamba watatakiwa kulipa kiasi kikubwa cha fedha kuliko klabu nyingine kubwa.
Katika tukio jingine, mmiliki wa Brighton, Tony Bloom amesema kwamba ni ngumu sana kushusha daraja timu ikiwa mechi zilizobaki hazitamalizika. Bado haijulikani msimu utamalizika vipi, licha ya kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki jana.
“Itakuwa ngumu sana kushusha daraja klabu, hasa ikiwa msimu wote haujamalizika,” akasema Bloom na kuongeza kwamba hawatakubaliana na hali hiyo kwa sababu vigezo na masharti hayatakuwa yametimizwa.
Klabu nyingi zinaona kwamba ikifika mwishoni mwa mwezi Juni iwe mwisho wa msimu bila kujali kama janga la virusi vya corona litakuwa limemalizika. Brighton wanashika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi hiyo wakati Liverpool wanaongoza ligi na wanachukuliwa kama mabingwa wateule.
Ligi inaweza kumalizika kwa kufutwa msimu wote bila kombe kutolewa, kusubiri janga la Covid-15 kumalizika au wachezaji kupimwa na wakiwa timamu bila maambukizi pamoja na maofisa wanaoingia uwanjani wacheze bila watazamani.