in , , ,

ARSENAL v. MANCHESTER UNITED

 

Kesho Jumapili Arsenal watakuwa wenyeji wa Manchester United kwenye mchezo wa mzunguko wa nane wa Ligi Kuu ya England. Washika bunduki hao kutoka London wanashikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wa EPL wakiwa na alama 13 wakati United ndio vinara wa ligi hiyo baada ya kukusanya alama 16.

Vijana wa Arsene Wenger wanakwenda kwenye mchezo huo wakiwa wametoka kupoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hapo Jumanne dhidi ya Olympiakos ndani ya uwanja wao wa nyumbani kwa mabao matatu kwa mawili. United wao walipata ushindi wa 2-1 kwenye mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Wolfsburg siku ya Jumatano.

Pengine kumbukumbu ya matokeo hayo ya Ligi ya Mabingwa inamuweka mwalimu wa Arsenal kwenye presha huku ikimuweka Louis van Gaal wa Manchester United katika hali ya utulivu na kujiamini kuelekea mchezo baina yao hapo kesho.

Kikosi cha Wenger kina jumla ya majeruhi watano ambao ni Jack Wilshere, Thomas Rosicky, Danny Welbeck, Mikel Arteta na Laurent Koscielny. Kuna wasiwasi kuwa huenda Petr Cech na Mathieu Flamini nao pia watashindwa kutumika kwenye mchezo wa kesho kutokana na majeraha. Kwa upande wa Manchester United wachezaji walio majeruhi ni walinzi Luke Shaw na Marcos Rojo pekee.

Tangu United ilipoanza kufundishwa na Louis van Gaal timu hizi zimekutana mara tatu ambapo kila timu imeshinda mchezo mmoja na mchezo wa mwisho uliisha kwa sare ya bao moja kwa moja. Hata hivyo mchezo ambao Arsenal walishinda ulikuwa mchezo wa Kombe la FA na si EPL.

Timu zinaweza kupangwa hivi
Timu zinaweza kupangwa hivi

Mara ya mwisho Arsenal kupata matokeo ya ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Manchester United ilikuwa tarehe 1 Mei 2011 ambapo bao pekee la Aaron Ramsey lilitosha kuwapatia Arsenal alama zote tatu za mchezo huo. Baada ya mchezo huo timu hizi zimekutana mara nane kwenye EPL ambapo Manchester United wameshinda michezo mitano na michezo mitatu ilimalizika kwa sare.

Tukizigeukia takwimu za msimu huu zinaonyesha kuwa Arsenal wameshinda mchezo mmoja tu kati ya michezo mitatu ya EPL ambayo wamecheza kwenye dimba lao la Emirates ambapo kwenye mingine miwili walipoteza dhidi ya West Ham na wakatoa sare dhidi ya Liverpool.

Huenda takwimu hizo nazo zinawaongezea matumaini Manchester United ambao kwenye kila mchezo kati ya michezo yao mitatu ya mwisho ya EPL dhidi ya Liverpool, Southampton na Sunderland walifanikiwa kufunga mabao matatu.

Pia Arsenal ndio timu inayoongoza kwa wastani wa umiliki wa mpira msimu huu ikiwa na wastani wa asilimia 60 na pia inaongoza kwa wastani wa usahihi wa pasi ambapo ina asilimia 86. Kwa upande wa mashuti Arsenal ni vinara pia ambapo wana wastani wa mashuti 21 kwa mchezo mmoja.

United wao kitakwimu ndio timu yenye ulinzi mkali zaidi msimu huu ambapo wameruhusu mabao machache kuliko timu yoyote sawa na Tottenham walioruhusu mabao matano pia kwenye michezo saba.

Nyota wa kutazamwa zaidi kwa upande wa Arsenal hapo kesho ni Alexis Sanchez ambaye wiki iliyopita alifunga hat-trick dhidi ya Leicester City. Kwa upande wa Manchester United, Juan Mata ndiye mchezaji anayeng’ara zaidi kwa sasa baada ya kuonyesha kiwango safi kwenye michezo ya karibuni hasa mchezo wa Ligi ya Mabingwa ambao United waliibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Wolfsburg.

Advertisement
Advertisement

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

England yataja kikosi

Tanzania Sports

Arsenal wawanyonga Man U 3 – 0