Arsenal wamefika robo fainali ya Kombe la FA baada ya kuwapiga Middlesbrough kwa mabao mawili ya mapema na kuwatupa nje.
Alikuwa mshambuliaji Mfaransa, Olivier Giroud aliyetupia mabao hayo katika dakika ya 27 na ya 29, katika mechi ambayo beki mpya wa kati, Gabriel Paulista kutoka Hispania alicheza kwa mara ya kwanza.
Arsenal walionesha mchezo mzuri dhidi ya timu waliowafunga Manchester City na kuwatupa nje ya michuano.
Santi Cazorla aliichambua ngome ya maadui na kumpa mpira beki aliyepanda Kieran Gibbs aliyempasia Giroud kwa bao la kwanza.
Giroud aliongeza la pili zuri kwa shuti maridhawa baada ya Boro kutokuwa makini kwa mpira wa kona, huku macho ya wengi yakisubiri mechi baina ya Preston wanaowakaribisha Manchester United jioni ya Jumatatu hii.
Wachezaji wote 11 wa Arsenal waligusa mpira kabla ya Giroud kufunga bao, ambapo Paulista hakuwa na kazi nzito, huku golini akirejea kipa namba moja aliyezoeleka, Wojciech Szczesny.
Boro walifika hatua hii baada ya kuwapiga Man City 2-0 na kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alisema walikuwa wakiingia kwenye mechi hiyo kw auangalifu, huku yule wa Chelsea akitaka kuona Arsenal wakifungwa, ili waungane nao nje ya mashindano hayo.
Katika mechi nyingine, Aston Villa walio chini ya kocha mpya Tim Sherwood aliyepata kufanya kazi Tottenham Hotspur walifanikiwa kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Leicester.
Bradford wakawasambaratisha Sunderland 2-0 na kuzidi kumpa hali mbaya kocha wa Sunderland, Gus Poyet aliyekuwa amewazuia wachezaji wake kutoa pasi za ama nyuma au za pembeni.
Comments
Loading…