Mabingwa watetezi wa Kombe la FA, Arsenal wamebanwa na Hull kwenye
mechi ya 16 bora kwa kwenda suluhu.
Katika mechi ambayo Arsenal walitawala kwa kila hali wakicheza
nyumbani, kikwazo kikubwa kilikuwa kipa wa Hull, Eldin Jakupovic.
Kwa matokeo hayo, Arsenal watatakiwa kusafiri kwenda kucheza na Hull
nyumbani kwao katika mechi ambayo, lazima, mshindi atapatikana.
Washika Bunduki wa London waliona kwamba walikataliwa penati mbili
ambazo huenda zingewapa ushindi, kutokana nakuchezewa vibaya kwa Theo
Walcott na Danny Welbeck waliotoka kwenye majeruhi hivi karibuni.
Kipa Jakupovic aliwaokoa Hull ambao walionekana wangesalimu amri kama
walivyofanya msimu uliopita kwenye mashindano kama haya. Moja ya hayo
ni kutungua mpira wa adhabu ndogo wa Joel Campbell ukaishia kugonga
mwamba.
The Tigers, jina jingine la Hull, walitengeneza nafasi chache za
kufunga lakini walilinda lango lao na kumweka katika hali ngumu kocha
Arsene Wenger aliyekuwa akiwaongoza Arsenal katika mechi yake ya 100
kwenye michuano hii akiwa bosi wao.
Hull wanaofundishwa na Steve Bruce na ambao wanaongoza Ligi Daraja la
Kwanza (Championships) nao hawakufurahia matokeo, kwani wamekatizwa
mserereko wa ushindi katika mechi 14 zilizopita.
Timu mbili hizi zilikutana kwenye fainali ya Kombe la FA 2014 na
raundi ya tatu msimu uliopita; zote Arsenal wakishinda.
Ni wazi kwamba kipaumbele kwa Arsenal kipo kwingine, wakiwa pointi
mbili tu nyuma ya Leicester wanaoongoza Ligi Kuu ya England (EPL).
Jumanne hii wana kibarua kingine cha kuwakaribisha Barcelona katika
mechi ya mkondo wa kwanza ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Arsenal hawajapata kuvuka hatua hii katika misimu mitano iliyopita, na
katika mechi dhidi ya Hull, mchezaji wao muhimu katika kutengeneza na
kufunga mabao, Mesut Ozil alipumzishwa, wakati Olivier Giroud na
Alexis Sanchez ambao ni muhimu pia walianzia benchi hadi dakika za
mwisho mwisho.
Hii ni mara ya kwanza kwa Hull kutoruhusu Arsenal kuwafunga walau bao
moja katika mechi 17 walizokutana kwenye mashindano yote, na mara ya
mwisho ilikuwa 1915. Jumamosi hii Arsenal walipiga mashuti 24 ambayo
hayakuzaa bao lolote, mengi kuliko mechi yoyote msimu huu katika
mashindano yote.
Katika mechi nyingine, Reading waliwakandamiza West Bromwich Albion
kwa mabao 3-1 na kuvuka, Watford wakapoteza 0-1 kwa Leeds wakati
Bournemouth wakazidiwa nguvu 0-2 na Everton.