in , , ,

Arsenal matawi ya juu

*Wanashindana na klabu nyingine kubwa
*Puma, Emirates wawapa jeuri ya fedha

Ule unyonge ambao Arsenal walizoea kuwa nao unaanza kupotea, kutokana na jinsi wanavyojiimarisha kiusajili na kupata dili za nguvu kwenye udhamini.

Hilo linaonekana miongoni mwa wamiliki, viongozi, kocha, wachezaji na hata washabiki wa klabu hiyo waliosambaa kwa wingi pembe zote za dunia.

Mwanahisa wa pili kwa nguvu ya hisa, Alisher Usmanov alisema majuzi kwamba Arsenal inatakata na akasema misimu ya kuzoa mataji inarudi tena, akisema kwamba klabu ilikuwa inaumizwa na madeni na mzigo mkubwa wa kujenga uwanja wa pili kwa ukubwa miongoni mwa klabu za Ligi Kuu, Emirates.

Mawazo yake yanafanana na ya kocha Arsene Wenger, anayesema kwamba katika miaka miwili hii wapo vizuri, na nguvu hiyo inaonekana hata kwenye usajili, ambapo wanakaribia kutamba sawa na klabu nyingine kubwa.

Baada ya kumsajili Mesut Ozil msimu uliopita na Alexis Sanchez kiangazi hiki kwa ajili ya msimu ujao, Wenger anaamini kwamba wapo juu, akiongeza kwamba ingekuwa miaka mitano iliyopita, wangewapoteza wachezaji wa aina ya Ozil na Sanchez.
20140416-145957

Ni wakati huu ambapo tunasikia tambo za Arsenal kupigana vikumbo na klabu kama Manchester United, Chelsea na nyinginezo na hata kufikiria kuchukua wachezaji huko, kwani wanayo jeuri ya fedha, hasa baada ya kuingia mkataba mpya wa mamilioni na Puma.

Mkataba na kampuni hiyo kubwa umewezesha fedha kutiririka klabuni hapo, ambapo Wenger anaruhusiwa kutumia zaidi ya pauni milioni 100 msimu huu kwa ajili ya kununua wachezaji, lakini kama kawaida anafanya hivyo kwa umakini mkubwa na taratibu.

Usajili unaosifika zaidi msimu huu ni wa Sanchez, lakini pia Wenger alisonga mbele haraka kuziba pengo la Bacary Sagna aliyehamia Manchester City kwa kumchukua Mathieu Debuchy wa Newcastle na ambaye anacheza beki ya kulia Timu ya Taifa Ufaransa, akimweka benchi Sagna. Hapo Arsenal imelamba dume, maana ni mdogo kiumri.

Tayari Theo Walcott ameonya timu pinzani, akisema akicheza na Sanchez basi watarajie maafa makubwa, ikizingatiwa pia Olivier Giroud yupo sawa na viungo mahiri  Özil, Santi Cazorla na Aaron Ramsey ambaye kama si kuumia si ajabu leo Arsenal wangekuwa mabingwa wa England.

Wenger sasa anajitapa kwa kuwa na jeshi kubwa na zuri la viungo, mawinga na washambuliaji katika watu kama Tomasz Rosicky, Cazorla, Jack Wilshere, Özil, Ramsey, Podolski, Walcott, Oxlade-Chamberlain, Giroud Sanchez na Joel Campbell lakini pia golini kuna makipa wawili wazuri sana, David Ospina na Wojciech Szczęsny.

Kwa hiyo ‘Profesa’ Wenger anaingia kwenye msimu huu akiwa ameshaondoa kiwingu cha kukosa makombe kwa miaka tisa kwa kutwaa lile la FA lakini pia anajiandaa na kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Anatunishiana misuli na makocha wengine wakubwa kama Louis van Gaal anayeijenga upya Manchester United, Manuel Pellegrini anayewaongoza Man City kutetea ubingwa na Jose Mourinho aliyedai Wenger amebobea katika kufeli.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Tetesi za usajili leo …

Celtic warejeshwa Ligi ya Mabingwa