*Chelsea waendelea kukamua
Arsenal wamefanya maangamizi kwa kuwapiga Liverpool 4-1 kwenye mechi muhimu ya Ligi Kuu ya England (EPL) na kuchupa hadi nafasi ya pili.
Wakicheza nyumbani, The Gunners walifunga mabao matatu katika dakika nane za kipindi cha kwanza na kuwanyamazisha kabisa Liverpool.
Alikuwa beki chipukizi wa pembeni, Hector Bellerin aliyefungua kitabu kwa bao kwenye mechi iliyowafanya Arsenal kuwa na ushindi wa mechi 10 kati ya 11 zilizopita za ligi.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers alisema kwamba matumaini yao ya kufuzu kwa mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) ni kama yamekufa.
Mabao mengine ya Arsenal yalitiwa kimiani na Mesut Ozil, Alexis Sanchez na Olivier Giroud ambaye sasa amefunga mabao 10 katika mechi kama hizo.
Raheem Sterling aliyekataa kusaini mkataba mpya na Liverpool huku akitajwa kwamba anatakiwa na Arsenal, alianza kucheza kama mshambuliaji wa kati wa Liver lakini hakufanikiwa kufanya vyema.
Hata hivyo, alipambana na kufanikiwa kupata penati dakika za mwisho, ambayo ilifungwa na Jordan Henderson.
Katika mechi nyingine vinara wa EPL, Chelsea waliendeleza makamuzi yao kwa kuwafunga Stoke 2-1.
Katika mechi ambayo mshambuliaji wao mahiri Diego Costa alicheza kwa dakika 10 tu na kulazimika kutoka nje kwa kuumia, Chelsea wameacha wanaowafuata kwa pengo la pointi saba.
Mabao ya Chelsea yalifungwa na Eden Hazard kwa penati na Loic Remy na kuwafikisha kwenye pointi 70.
Kwenye mechi nyingine, Manchester United waliwafunga Aston Villa 2-1, Everton wakashangaza kwa kuwafunga Southampton 1-0 na Leicester wakawazidi nguvu West Ham kwa kuwafunga 2-1.
Kwingineko, Swansea waliwalalia Hull 3-1 na QPR wakaona mwezi kwa kuwafunga West Bromwich Albion 4-1.
Comments
Loading…