*Man United wapigwa tatu bila
Mtanange mkubwa katika Jiji la London umemalizika kwa suluhu baina ya Arsenal na Chelsea.
Kama ilivyotarajiwa, Chelsea walijilinda zaidi kuliko kushambulia na Arsenal walikosa nafasi kadhaa katika kipindi cha pili.
Washabiki wa Arsenal waliwazomea Chelsea wakisema kwamba walikuwa wakifanya mchezo udorore kwa jinsi walivyokuwa wakibana nyuma, lakini kocha wao, Jose Mourinho alidai walitoa somo juu ya ulinzi.
Wachezaji wa Chelsea walishangilia suluhu hiyo kana kwamba walikuwa wameshinda, hasa nahodha wao, John Terry.
Arsena sasa hawajaweza kuwafunga Chelsea katika mechi 13 dhidi ya Mourinho na sasa Chelsea wanakaribia kuutwaa ubingwa wa England, wakati Arsenal wakianguka hadi nafasi ya tatu.
MANCHESTER UNITED HOI
Manchester United kwa upande mwingine waliangukia pua mbele ya Everton kwa kukung’utwa 3-0 kwenye dimba la Goodison Park.
Vijana wa Louis van Gaal walishindwa kabisa kufanya vyema mchezoni wakacharazwa kama wamesimama.
Mabao ya wenyeji yalifungwa na James McCarthy, John Stones na Kevin Mirallas, ambayo yangeweza kuzuilika kama Mashetani Wekundu wangelinda vyema.
Huu ulikuwa ushindi mkubwa zaidi wa Everton dhidi ya Manchester United katika muda wa miaka 23.
MATOKEO MENGINE YA LIGI KUU
Katika mechi nyingine za wikiendi hii, Manchester City walipata ushindi wa 3-2 dhidi ya Aston Villa na kupanda hadi nafasi ya pili lakini wana mechi moja zaidi ya Chelsea na Arsenal.
Southampton walikwenda sare ya 2-2 na Tottenham Hotspur, Burnley wakalala kwa Leicester, Crystal Palace wakalala 2-0 kwa Hull na Newcastle wakalala 2-3 mbele ya Swansea.
Kwenye mechi nyingine Queen Park Rangers (QPR) walikwenda suluhu na West Ham, Stoke wakatoka sare ya 1-1 na Sunderland na West Bromwich Albion wakawalazimisha suluhu Liverpool.
Kwa matokeo hayo, Chelsea wanaongoza ligi kwa alama 77 wakifuatiwa na Man City wenye 67 sawa na Arsenal wakati Man United wanazo 65.
Liverpool wanashika nafasi ya tano kwa alama 58 sawa na Spurs wakifuatiwa na Southampton wenye 57.
Swansea, Stoke na Everton wanafunga 10 bora wakati Burnley wapo mkiani na alama 26, QPR wanazo 27 na Sunderland 30 hivyo kuwa katika hatari ya kushuka daraja.
Comments
Loading…